Waandamanaji wataka kuachiwa Deniz Yucel Uturuki
1 Machi 2017Mjini Berlin karibu magari 100 na baiskeli 19 zilishiriki katika maandamano hayo kote katika mji huo mkuu wa Ujerumani, kama sehemu ya kile kinachojulikana kama " Juhudi za kupigania kuachiwa huru Deniz". Baadae waandamanaji wakakusanyika kwenye Ubalozi wa Uturuki kudai Yucel aachiwe huru .
Baadhi ya mabango yalikuwa na maandishi " Uhuru kwa waandishi wote waliokamatwa Uturuki".
Miongoni mwa waliohutubia ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Kijani cha Ujerumani Cem Ozdemir ambaye alitoa wito wa kuachiwa waandishi habari na wanaharakati wanaopigania demokrasia ambao kwa wakati huu wako gerezani.
Maandamano yalifanyika pia katika miji ya Cologne, Frankfurt na Munich.
Awali waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel alimwita balozi wa Uturuki kwenye Wizara ya kigeni mjini Berlin na kuzungumzia kisa cha Yucel. Baada ya mazungumzo yao Gabriel alisema, kuwekwa ndani Yucel nchini Uturuki ambapo anaweza kubakia hadi miaka mitano kabla ya kuachiwa huru au kufikishwa mahakamani, kumesababisha mvutano mkubwa katika uhusiano wa nchi hizo mbili na kwamba na moja wapo ya mitihani mikubwa ya wakati huu.
"Uamuzi huu sio tu wakushangaza pia si wa lazima na usio na kipimo. Mtu anayefanyakazi yake ya uandishi habari sio tu Ujerumani bali pia Uturuki, ana haki za kinga na uhuru wakutoa maoni, " alisema waziri Gabriel.
Amri "chungu na ya kuvunja moyo"
Yucel ambaye ni mwandishi habari mwakilishi wa gazeti la Ujerumani Die welt na mwenye uraia pacha- wa Ujerumani na Uturuki alikamatwa Februari 14 na kuwekwa rasmi kizuizini siku 13 baadae, hatua iliokosolewa vikali nchini Ujerumani. Kansela Angela Merkel aliitaja amri hiyo ya mahakama kuwa "chungu na yenye kuvunja moyo".
Rais Joachim Gauck kwa upande wake alitamka", Sisi nchini Ujerumani tunashindwa kufahamu kwanini kuna haja ya kuvishambulia vyombo vya habari". akaongeza kwamba kile kinachotokea Uturuki hivi sasa kinazusha shakashaka iwapo kweli Uturuki inataka kubakia kwenye utawala wa kisheria.
Mwandishi huyo wa habari aliandika ripoti mwezi Septemba kuhusu kuandamwa na vitisho vya mitandaoni dhidi ya wanaoikosoa serikali, kukitumiwa anuwani za baruapepe za Waziri wa nishati Berat Albayrak ambaye ni mkwewe Rais Recep Tayip Erdogan.
Baruapepe tatu zilichapishwa na mtandao wa ufichuzi wa Wikileaks na kundi moja la upekuzi wa mitandao nchini Uturuki. Yucel anatuhumiwa kwa kueneza propaganda za Chama cha wafanyakazi cha Wakurdi -PKK- kilichopigwa marufuku na kile cha kiongozi wa kidini Fethullah Gulen ambaye serikali ya Uturuki inamtuhumu kuwa nyuma ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa Julai mwaka jana 2016.
Makundi yote mawili yanatajwa na serikali ya Uturuki kuwa ya kigaidi. Leo Umoja wa Ulaya umeitaka Uturuki kufuata utawala wa kisheria. Kamishna anayehusika na kutanuliwa kwa Umoja huo Johannes Hahn aliliambia gazeti la Welt kwamba, Umoja wa Ulaya unashtushwa na idadi kubwa ya waandishi habari waliokamata na kuwekwa ndani nchini Uturuki.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, afp,dpa
Mhariri:Yusuf Saumu