1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wamtaka kiongozi wa Hong Kong kujiuzulu

Admin.WagnerD1 Oktoba 2014

Viongozi wa wanafunzi wa vyuo walioanzisha maandamano Hong Kong ya kutaka mageuzi ya kidemokrasia wameonya leo kuwa iwapo kiongozi wa Hong Kong, Leung Chunying, hatajiuzulu ifikapo kesho, watachukua hatua zaidi

https://p.dw.com/p/1DOMy
Picha: Reuters/Tyrone Siu

Viongozi wa wanafunzi hao wameonya kuwa miongoni mwa hatua watakazozichukua ni kuyakalia majengo muhimu ya serikali suala ambalo litauchochea hata zaidi mzozo huo na kusababisha makabiliano mengine makali kati ya waandamanaji na polisi.

Naibu katibu wa chama cha wanafunzi wa chuo kikuu cha Hong Kong Lester Shum amesema wataikaribisha fursa ya afisa wa serikali kuu ya China kuja kuzungumza nao katika ukumbi ambao wameweka kambi tangu Jumapili.

Waandamanaji hawataki mazungumzo na Leung

Hata hivyo, Lester amesema hawatafanya mazungumzo na Leung kwa sababu aliamrisha polisi iwarushie mabomu ya kutoa machozi mwishoni mwa juma lililopita na wanachokitaka kutoka kwake ni kujiuzulu tu.

Kiongozi wa Hong Kong Leung Chun Ying
Kiongozi wa Hong Kong Leung Chun YingPicha: Alex Ogle/AFP/Getty Images

China hii leo imesisitiza kuwa uchaguzi wa kumchagua kiongozi wa Hong Kong lazima utaendeshwa kuambatana na sheria zilizopo na kukariri msimamo wake wa awali kuwa maandamano yanayoendelea Hong Kong ni kinyume na sheria.

Gazeti rasmi la serikali ya China, People Daily, limesema maandamano yasiyo halali yameathiri vibaya shughuli za kawaida za kijamii, uchumi na njia za watu kujipatia riziki na kuonya iwapo yataruhusiwa kuendelea, athari zake zitakuwa kubwa mno.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya China na la kimataifa la Amnesty International yameripoti leo kuwa kiasi cha watu 20 wanazuiwa na maafisa wa usalama huku kiasi cha wengine sitini wakichukuliwa ili kuhojiwa nchini China kwa madai ya kuunga mkono maandamano ya Hong Kong.

Maandamano yaungwa mkono kimataifa

Maandamano hayo yamevutia hisia mbali mbali kutoka jumuiya ya kimataifa. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema atamuita balozi wa China nchini mwake kuzungumzia mzozo huo akiongeza ni muhimu kwa watu wa Hong Kong kuwa na haki ya kumchagua kiongozi wao.

Miongoni mwa waandamanaji wa Hong Kong
Miongoni mwa waandamanaji wa Hong KongPicha: Reuters/Carlos Barria

Mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel askofu mstaafu wa kanisa la Kianglikana Desmond Tutu amewaunga mkono waandamanaji hao na kuwashutumu askari kwa kujaribu kuwakandamiza.

Tutu ameitaka China kutoogopa sauti ya wananchi badala yake iheshimu wanachokitaka. Huku Gavana wa zamani wa Hong Kong, Chris Patten, akitoa wito kuwepo mazungumzo ya kweli kuhusu haja ya kutanuliwa kwa demokrasia Hong Kong, badala ya kutumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha.

Rais wa Taiwan, Ma Ying jeou, amesema serikali yake inayaunga mkono maandamano hayo na kuitaka serikali ya China kutimiza ahadi yake kuwa itaipa Hong Kong uhuru kamili wa kuendesha mambo yake au ijikute katika hatari ya kutengwa zaidi na Taiwan.

Mwandishi: Caro Robi/dpa/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Khelef