1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wamtaka kiongozi wa Hong Kong ajiuzulu

Admin.WagnerD30 Septemba 2014

Waandamanaji wanaodai mageuzi ya kidemokrasia Hong Kong wamemtaka kiongozi wa Hong Kong, Leung Chun Ying, kukutana nao hii leo la sivyo watachukua hatua zaidi za kuonyesha ghadhabu zao

https://p.dw.com/p/1DNrx
Picha: Reuters/B. Yip

Hatua ya Leung Chun Ying kukatalia mbali matakwa ya maelfu ya waandamanaji wanaotaka mfumo mpana zaidi wa demokrasia na kufanyiwa mageuzi sheria za uchaguzi ili kuipa Hong Kong uhuru zaidi wa kujitawala kwa njia ya kidemokrasia,imeondolea mbali matumaini ya kuumaliza mzozo huo wa siku kadhaa ambao umekwamisha shughuli katika mji huo.

Kiongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu walioanzisha maandamano hayo Alex Chow amesema iwapo Leung hatajitokeza katika ukumbi wa umma walipokita kambi ifikapo saa sita za usiku, basi hakutakuwa na budi bali watu zaidi kujiunga na maandamano hayo.

Waandamanaji kuchukua hatua zaidi

Chow amesema wanafunzi hao wanapanga kuchukua hatua zaidi kuweza kueleweka katika ajenda zao za kutaka mageuzi ikiwemo kuyatanua maandamano hayo kote Hong Kong,kushinikiza mgomo wa wafanyakazi na kuyakalia majengo ya serikali.

Kiongozi wa Hong Kong Leung Chun Ying
Kiongozi wa Hong Kong Leung Chun YingPicha: Alex Ogle/AFP/Getty Images

Wanafunzi hao walikuwa wanamtaka Leung kujiuzulu,jambo ambalo amelikatalia mbali.Serikali kuu ya China hairidhii kuwepo mazungumzo ya maridhiano na waandamanaji hao kwa kuhofia kwa kufanya hivyo,kutawapa nguvu makundi mengine yanayotaka kujitenga kutoka China.

Waandamanaji hao wanataka kubatilishwa kwa uamuzi uliofanywa na serikali ya China mwezi uliopita kuwa jopo linaloungwa mkono na serikali ndilo litawachuja wagombea wa wadhifa wa kiongozi wa Hong Kong katika uchaguzi unaotarajiwa mwaka 2017, hatua ambayo inaonekana kukengeuka ahadi ya awali kuwa kiongozi atachaguliwa kwa njia huru na ya haki na wote.

Watu zaidi wanatarajiwa kujiunga na maandamano hayo makubwa hapo kesho siku ambayo China inasherehekea sikukuu ya kitaifa na serikali imetangaza kuwa imefutilia mbali hafla ya kufyatua fataki kuadhimisha sherehe hizo.

Wanaharakati wakamatwa China

Maafisa wa China wamewakamata wanaharakati kadhaa na kuidhibiti mitandao miongoni mwao ni mwanaharakati Wang Long anayeishi mji wa Shenzhen unaopakana na Hong Kong.

Wanafunzi wakiandamana Hong Kong na picha ya kumdhihaki Leung Chun Ying
Wanafunzi wakiandamana Hong Kong na picha ya kumdhihaki Leung Chun YingPicha: XAUME OLLEROS/AFP/Getty Images

Mwanaharakati huyo amekamatwa kwa kusambaza ujumbe kuwa anaunga mkono maandamano ya Hong Kong na jaribio lake la kuzishatiki idara za serikali ya mitaa miongoni mwa masuala mengine.

Polisi mjini Shanghai pia imemkamata kwa muda mwanaharakati Shen Yanqiu alipokuwa akirejea kutoka mji wa Guanzhou lakini baadaye wakamuachilia wakimpiga marufuku kutosafiri Hong Kong wala Beijing.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imesema inafuatilia kwa karibu maandamano hayo na kusisitiza kuwa waandamanaji wana haki ya kuandamana kwa amani. Ufaransa imewaonya raia wake walioko Hong Kong kuchukua tahadhari na kuepuka sehemu kuliko na mikusanyiko.

Kampuni kubwa ya kuuza bidhaa za urembo ya L'Oreal imetangaza imefutilia mbali safari zake za kibiashara Hong Kong hadi tarehe sita mwezi ujao kutokana na maandamano hayo.

Mwandishi:Caro Robi/

Mhariri:Josephat Charo