1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mjadala wa kujadili mswada huo wa sheria umeahirishwa

Faiz Musa12 Juni 2019

Maafisa wa polisi wametumia risasi za mpira na gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji katika viwanja vya bunge la Hong Kong wanaopinga mswada wa sheria wa kuwapeleka washukiwa wa uhalifu China Bara.

https://p.dw.com/p/3KGYI
Hong Kong Demonstration gegen das Zulassen von Auslieferungen nach China
Picha: Getty Images/AFP/D. de la Rey

Muda wa mwisho uliotolewa na waandamanaji hayo kwa serikali kuachana na mswada huo ulikamilika asubuhi hivyo kuanza kuziziba barabara za kulekea bungeni na kusababisha mjadala uliokuwa ufanyike bungeni kujadili mswada huo kuahirishwa. Bunge hilo liko na wabunge wengi ambao ni watiifu kwa serikali ya China ambayo inaunga mkono mswada huo wa sheria.

Polisi walikabiliana na waandamanaji hao ambao walikuwa wakipiga fujo wakitamka kauli mbiu ya Vuguvugu la Mwavuli, wakiwa  wamevaa nguo nyeusi na kuwarushia polisi miavuli na vyuma huku wakiziba barabara. Polisi walijibu kwa kuwarushia maji ya kuwasha na kuwaondoa katika sehemu moja ya bunge walilolizingira.

Hong Kong | Protest gegen Auslieferungen nach China & Ausschreitungen
Maafisa wa polisi wakiwarushia waandamanaji vitoa machozi, Hong KongPicha: Reuters/A. Perawongmetha

Mkuu wa polisi wa Hong Kong, Stephen Lo, aliwateteta maafisa wa polisi akisema walilazimika kuwatawanya waandamanaji pale walipojaribu kujilazmisha kuingia bungeni huku wakitumia silaha hatari na kuwarushia polisi vyuma na matofali. Waandamanaji hao ni umoja wa aina yake unaojumuisha raia, wafanyabiashara, mawakili, wafanyakazi, makundi ya dini na miungano ya wanafunzi wanaopinga sheria hiyo ambayo lau itapita basi jimbo la Hong Kong litaweza kuwapeleka washukiwa wa uhalifu katika China bara kufunguliwa mashtaka.

Hong Kong haitaki kuingiliwa mambo yake ya ndani

Mataifa ya Magharibi yanapinga mipango hiyo huku Beijing ikiunga mkono. Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May ameliambia bunge la Uingereza kwamba wana wasiwasi na mswada huo kwa kuzingatia kwamba Waingereza wengi wako Hong Kong kwa hivyo mswada huo wa sheria unafaa kwenda sambasamba na azimio la pamoja la China na Uingereza la haki na uhuru.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China, Geng Shuang, aliikosoa Marekani na kuitaka itahadhari na matamshi inayotoa juu ya mswada huo.

"Tumekuwa tukikariri kwamba mambo ya Hong Kong ni maswala ya China. Hakuna nchi, mshirika wala mtu aliye na haki ya kutuingilia. Ningependa kusisitiza kwamba serikali kuu ya China itaendelea kuiunga mkono Hong Kong katika kutekeleza marekbisho haya ya sheria," alisema Geng Shuang.

Viongozi wa Hong Kong wanasema sheria hiyo itasaidia kuzuia mji huo kutumiwa kama hifadhi ya wakimbizi na wala haiwalengi wakosoaji wa serikali ya China. Raia hawaamini hayo na wanadai China inataka kuua uhuru wa kipekee na tamaduni za Hong Kong kinyume cha makubliano ya miaka hamsini baina ya koloni la Hong Kong, Uingereza na China.

(RTRE/AFPE)