Waandamanaji wa Hong Kong washambuliwa
22 Julai 2019Kundi la waandamanaji waliokuwa wakitoka katika maandamano ya kuipinga serikali Jumapili, limevamiwa na watu waliovalia tishati nyeupe wakiwa wamebeba marungu na paipu za chuma.
Vidio iliyorushwa mubashara kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook imeonyesha watu waliokuwa wakipiga mayowe, huku washambuliaji wakiwapiga waandamanaji pamoja na waandishi habari na kusababisha umwagaji damu katika kituo cha treni cha Yuen Long na wengine wakiwa ndani ya treni.
Wahudumu wa afya wamesema watu 45 wamejeruhiwa wakati wa mashambulizi hayo, mmoja wao yuko katika hali mbaya na watano wengine wamepata majeraha mabaya.
Wakosoaji wanawalaumu maafisa wa polisi kwa kuchelewa kwa zaidi ya saa moja kufika kwenye eneo la tukio, licha ya kupigiwa simu kadhaa na watu waliokuwa wakishambuliwa. Polisi pia walishindwa kuwatia mbaroni washambuliaji hao, ambao walibakia mitaani karibu na kituo hicho cha treni hadi Jumatatu asubuhi.
Baadhi ya washambuliaji hao waliovalia tishati nyeupe walionekana baadae wakiondoka ndani ya magari yenye nambari za usajili za China Bara.
Regina Ip, mwanasheria anaeegemea upande wa China Bara na mwanachama wa Baraza Kuu la Hong Kong amelaani maandamano hayo.
"Vitendo vya namna hii, vinavyopinga mamlaka ya serikali kuu na utaratibu wa 'nchi moja, mifumo miwili' ni hatari sana kwa ustawi wa watu wa Hong Kong. Mwishoni mwa siku ni vijana ambao wataathirika zaidi iwapo mafanikio na utulivu wa Hong Kong utaharibiwa, " amesema Regina.
Polisi watawanya maandamano
Huku hayo yakijiri, maafisa wa polisi walikuwa wakipambana na waandamanaji wengine katikati ya eneo la kibiashara la jiji la Hong Kong. Polisi wa kuzima maandamano walitumia mabomu ya kutoa machozi pamoja na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji hao, masaa machache baada ya baadhi ya waandamanaji kurusha mayai dhidi ya jengo la kiserikali linaloiwakilisha China Bara mjini humo.
Hong Kong imetumbukia katika mgogoro mbaya zaidi kushuhudiwa katika historia yake ya miaka ya hivi karibuni. Kwa wiki kadhaa kumekuwa kukishuhudiwa maandamano ya vurugu, yanayowagonganisha maafisa wa polisi na waandamanaji.
Awali maandamano hayo yalichochewa na muswada wa sheria uliosimamishwa kwa muda, ambao ungepitishwa ungepelekea washukiwa kusafirishwa China Bara.
Lakini maandamano hayo sasa yamepanuka na kuwa makubwa zaidi, yakidai mageuzi ya kidemokrasia na haki ya kila mtu aliyetimiza umri kupiga kura.
Waandamanaji wameahidi kuendelea na vuguvugu lao hilo hadi pale madai yao yatakapotimizwa; ikiwa ni pamoja na uchunguzi huru dhidi ya polisi, msamaha kwa waandamnaji waliokamatwa, kufutwa kabisa kwa muswada uliochochea maandamano hayo, haki ya kila aliyetimiza umri kupiga kura na kujizulu kwa kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam.