Waandamanaji Kenya wavamia majengo ya bunge
25 Juni 2024Kutwa nzima, waandamanaji walikusanyika kwenye miji kadhaa kote nchini kupinga mswada wa fedha wa 2024 unaonuwia kuliongeza pato la taifa kupitia ukusanyaji wa kodi na ushuru.
Ving’ora vilirindima kote mjini na kuashiria uwepo wa maafisa wa usalama waliowarushia waandamanaji mabomu ya gesi ya kutoa machozi na pia kuwanyunyizia maji ya kuwasha. Watu wasiopungua watatu wanaripotiwa kupigwa risasi nje ya majengo ya bunge wakati polisi walipopambana na waandamanaji. Hayo ni kwa mujibu wa mkuu wa polisi katika kaunti ya Nairobi Adamson Bungei.
Waandamanaji kadhaa wauwawa Kenya
Kundi jengine la waandamanaji lililiangusha lango karibu na majengo ya Senate yaliyoko pembeni mwa Bunge. Lori moja la polisi nalo pia lilitiwa moto. Wabunge walilazimika kutoroka na kuokolewa pale waandamanaji walipopambana na maafisa wa usalama.Vurugu hizo ziliendelea hata baada ya alasiri na sehemu ya majengo ya bunge yalitiwa moto. Wabunge wa chama tawala waliendelea kushikilia kuwa huu ndio mkondo wa kufuata.
Wabunge wa upinzani wakutana na waandamanaji
Katika tukio ambalo halikutarajiwa, wabunge wa upinzani wa Azimio walitoka nje na kukutana na waandamanaji nje ya majengo ya bunge. Haya yalijiri baada ya mswada wa fedha wa 2024 kupigiwa kura 196 na kupingwa kwa kura 105. Kura tatu ziliharibika. Stewart Madzayo ni seneta wa kaunti ya kilifi na alikuwa nje ya majengo ya bunge na aliwaunga mkono waandamanaji.
Duru zinaeleza kuwa hospitali kuu ya Kenyatta imepokea majeruhi wasiopungua 40.Kwenye uwanja wa maandamano, matabibu wa kujitolea waliwapa majeruhi huduma ya kwanza kila ilipohitajika.
Rais wa Kenya asema yuko tayari kuzungumza na Gen-Z
Mashirika ya kiraia yameelezea wasiwasi wao baada ya baadhi ya wanaharakati kukamatwa na sasa hawajulikani waliko. Vurugu hizo zimeshuhudiwa pia kwenye miji miengine ya Mombasa, Kisumu, Nakuru, Eldoret, Kakamega na kwengineko.
Yote hayo yakiendelea, Rais William Ruto anahudhuria kikao cha amani cha Umoja wa Afrika mjini Naivasha alikosema kuwa ipo haja ya kufanya mageuzi haraka iwezekanavyo. Ifahamike kuwa mswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na rais ambaye pia ndiye mwenye uwezo wa kuurejesha kwa wabunge kufanyiwa kazi upya.
Thelma Mwadzaya
DW, Nairobi.