1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji 30 wauwawa nchini Iraq

26 Oktoba 2019

Kiasi waandamanaji 30 wameuwawa jana Ijumaa wakati wa wimbi jipya la maandamano ya umma yaliyofanyika dhidi ya serikali nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/3RygX
Irak Bagdad Proteste
Sehemu ya waandamanaji mjini BaghdadPicha: Reuters/K. al-Mousily

Hayo ni kulingana na Mjumbe wa Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Faisal Abdullah, ambaye amesema vifo hivyo vilitokea wakati polisi ilipofyetua risasi za moto na gesi ya machozi kutawanya waandamanaji.

Watu 8 waliuwawa kwenye mji mkuu Baghdad, wengine 18 katika miji ya Maysan na Dhi Qar, watatu mjini Basra na mtu mmoja aliuwawa kwenye jimbo la kusini la Muthanna.

Kulingana na Abdullah watu wengine zaidi ya 2,300 walijeruhiwa huku takriban majengo 50 ya serikali na ofisi za vyama vya siasa yaliyochomwa moto katika baadhi ya majimbo nchini Iraq.

Marufuku ya kutotoka nje imetangazwa kwenye majimbo ya  Dhi Qar, Basra, Muthanna na Wasit.

Maandamano yafanyika licha ya ahadi ya mageuzi 

Adil Abdul Mahdi
Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdul-MahdiPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Waandamanaji walianza kukusanyika kwenye medani ya Tahrir mjini Baghdad jana Ijumaa baada ya hotuba ya waziri mkuu Adel Abdel-Mahdi aliyoitoa kwa njia ya televisheni, ambayo aliitumia kutoa ahadi ya kufanya mageuzi na mipango ya kulifanyia mabadiliko Baraza lake la Mawaziri wiki ijayo.

"Kutaka serikali iangushwe bila kuwa na njia mbadala ya kikatiba kutaitumbukiza nchi kwenye machafuko " alisema Abdel-Mahdi.

Waandamanaji walipeperusha bendera za Iraq na kuimba kaulimbiu za kutaka kujiuzulu kwa serikali na Bunge.

Pia wanataka kufanyike mageuzi katika sheria za uchaguzi na tume mpya ya uchaguzi iundwe ikiwa na wajumbe walio huru.

Maandamano ya Ijumaa dhidi ya serikali yanafuatia maandamano kama hayo yaliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu ambayo yalisababisha vifo vya takriban raia 149 na maafisa 8 wa polisi.

Al-Sistani atoa wito pande zote kuepuka vurugu

Irak Bagdad Proteste
Picha: picture-alliance/AP Photo/H. Mizban

Wakati wa maandamano ya jana kiongozi mkuu wa kidini wa waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ali al-Sistani, alitoa wito kwa waandamanaji na vikosi vya usalama kujiuzia na vurugu.

Al-Sistani pia alikosoa ripoti ya hivi karibuni ya kamati ya serikali iliyokuwa inachunguza maandamano ya vurugu yaliyotokea mapema mwezi huu.

Alisema kamati hiyo "haikutoa ukweli wote kwa njia ya uwazi mbele ya umma".

Kamati hiyo ilibaini kuwa vikosi vya usalama vilitumia nguvu iliyopitiliza huku asilimia 70 ya vifo vya waandamanaji vilitokana na kupigwa risasi kichwani au kifuani.

Ripoti hiyo imewalaumu maafisa waandamizi wa usalama kwa kushindwa kuwasimamia maafisa walio chini yao lakini imesema hakukuwa na maelekezo yaliyotolewa na maafisa hao ya kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji.

Kadhalika imetaja majina kadhaa ya maafisa wa usalama inaoshauri wanapaswa kufukuzwa au kufunguliwa mashataka.

Maandamano nchini Iraq yamekuja mwaka mmoja tangu waziri mkuu Abdel-Mahdi kuchukua madaraka katika taifa hilo ambalo bado linaandamwa na matokeo ya  kampeni pana ya kijeshi ya kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislam, IS.