Waandamana Berlin kupinga chuki dhidi ya Uyahudi
1 Juni 2019Ni hatua inayofutia onyo lenye utata kuwa wayahudi hawatakuwa salama kuvaa kofia hizo, maarufu "Kippah" kwenye maeneo ya wazi nchini Ujerumani.
Kiasi waislamu 2000 wanatarajiwa kushiriki maandamano ya Al-Quds yaliyoandaliwa na makundi ya Waislam wenye misimamo mikali katika wakati ambapo chuki dhidi ya wayahudi inaongezeka nchini Ujerumani.
Siku ya Al-kuds ambayo huadhimishwa kuelekea mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhan imekuwa kitovu cha mvutano kati ya waarabu na Israel. Jana Ijumaa, rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliwarai wananchi wa Ujerumani kuwa ni lazima wapinge aina yoyote ya chuki dhidi ya Wayahudi.
Afisa anayehusika na kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi katika serikali ya Ujerumani Felix Klein, ametoa wito kabla ya maandamano kwamba kila mtu avae kofia ya Kiyahudi kama ishara ya mshikamano na Wayahudi na kupinga maandamano ya Al-Quds.
Ujerumani inakabiliwa na ongezeko la visa vya chuki dhidi ya Uyahudi.
Siku chache zilizopita hata hivyo alikosolewa vikali, pale alipowaonya Wayahudi dhidi ya kuvaa kikofia hicho hadharani nchini Ujerumani.
Katika mahojiano na DW, Klein amesema matamshi yake yalikuwa na lengo la kuanzisha mjadala nchini kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi. Kelin ameongeza kwamba lazima wananchi waonyeshwe kwamba chuki dhidi ya Wayahudi ni kitu kisichokubalika nchini Ujerumani.
Mwaka 1979 Iran ilianzisha siku ya Al-Quds ambalo ni neno la kiaarabu linalomaanisha mji wa Jerusalem ili kuwahimiza waislam kila mwaka kuurejesha mji wa Jerusalem baada ya kukaliwa kwa mabavu na Israeli mwaka 1967.
Afisa anayehusika na mapambano ya kupinga chuki dhidi ya Wayahudi katika jamii ya Wayahudi mjini Berlin Sigmount Koenigsberg amesema hayachukulii matamshi ya Klein kama kusalimu amri badala yake ni kama wito wa kuwa macho. Amesema "Ningetarajia aongeze kwamba kutafanyika kila linalowezekana ili kila Myahudi nchini Ujerumani uweze kuvaa kofia hiyo ya Kippa wakati wote.
Idadi ya matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi inapanda. Takwimu za kihalifu zinaeleza kwamba mwaka uliopita matukio 1799 yalihusiana na chuki dhidi ya Wayahudi.
Hii ni karibu na asilimia 20 zaidi ya mwaka 2017. Klein alitoa matamshi yake kwa msingi wa matukio haya ya kihalifu yakiongezeka katika jamii bila ya kudhibitiwa pamoja na matukio ya kikatili na kuwa chachu ya chuki dhidi ya Wayahudi.