Uganda yalaumiwa kutomfikisha mahakamani mwandishi maarufu
30 Desemba 2021Hii ni baada ya polisi kuthibitisha kuwa mwandishi huyo anazuiliwa kwenye mojawapo ya vituo vyake. Kankwenza anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, TEHAMA na mitandao ya kijamii.
Mwanzoni wanaharakati wa haki za binadamu pamoja na jamaa za mwandishi huyo Kakwenza Rukirabashaija hawakuwa na uhakika kuhusu kule aliko baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia Jumatano nyumbani kwake na watu waliojihami kwa silaha.
Soma zaidi: Wanaharakati walishutumu jeshi la Uganda kwa ukiukaji wa haki
Habari zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilielezea kuwa alitekwa nyara na mawakili wake walikuwa na jukumu la kuhakiki ukweli wa mambo. Sasa ni dhahiri kwamba yumo mikononi mwa vyombo vya usalama.
Naye msemaji wa polisi Fred Enanga amenukuliwa na vyombo vya habari akithibitisha kuwa mwandishi huyo mkosoaji mkubwa utawala kupitia fasihi na vitabu vyake anashikiliwa na vyombo vya usalama. Ameongeza kusema kuwa Kankwenza anakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya TEHAMA na mitandao ya kijamii lakini hakufafanua zaidi.
Ila kuna uvumi kwamba alimvunjia heshima kamanda wa majeshi ya nchi kavu Jenerali Muhoozi Kainerugaba kupitia kwa ujumbe wa Twitter aliosambaza.
Jenerali huyo pia ndiye mtoto wa Rais Yoweri Museveni. Hadi sasa mawakili wala ndugu wa mshukiwa hawajaruhusiwa kuwasiliana naye. Ni kwa ajili hii ndipo wanaharakati wanadai afikishwe mahakamani kama tayari amepatikana na hatia hiyo kuliko kuendelea kuzuiliwa.
Kitendo alichofanyiwa ni cha kikatili
Mwanaharakati mwingine wa haki za binadamu Nicholas Opiyo ametaja kitendo cha kukamatwa kwa Kakwenza Rukirabashaija mwenye umri wa miaka 33 kuwa cha kikatili kwa sababu waliomkamata walitumia nguvu za kupindukia na ndiyo maana wana wasiwasi kuhusu hali yake ya afya.
Mwandishi huyo wa kitabu kijulikanacho kama ‘Greedy Barbarian' alishinda tuzo la kimataifa la PEN mwezi Oktoba mwaka huu kutokana na kile kilichoelezewa kuwa ushupavu wake katika kuelezea kile anachoamini. Mwaka 2020 alikamatwa mara mbili bila kufikishwa mahakamani na hadi sasa shauri lake la kudai fidia halijasikilizwa katika Mahakama Kuu.