Vyombo vya dola vyatuhumiwa kuwaandama wapinzani
2 Machi 2016Katika mkutano mmoja wa hadhara hivi karibuni, Rais Yoweri Museveni aliutangaza mji wa Mbarara kuwa jiji katika mabadiliko, ambayo japo si makubwa sana, yanatoa fursa za ajira kwenye sekta ya umma kwa wapigakura wa huko.
Huku wanamuziki wakubwa wakiwatumbuiza maelfu ya wafuasi wa Museveni, wakosoaji wake wanasema huo ni mfano mwengine wa namna kiongozi huyo anavyotumia vibaya fedha za umma na nafasi yake serikalini kwenye kampeni za kusaka muhula mwengine madarakani baada ya miongo mitatu ya kuliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki, huku walimu wakiwa hawajalipwa mishahara na kliniki zikiwa hazina madawa.
"Kwa miaka 30 sasa, imekuwa ni sura ile ile, mfumo ule ule, uchumi ukiwa mikononi mwa wachache," anasema Steven mwenye umri wa miaka 53. "Ana vyombo vyote vya dola kumnunulia uchaguzi huu."
Hata hivyo, Museveni, ambaye serikali yake inakanusha kuponda fedha za umma kwenye kampeni za uchaguzi wa Februari 18, ameleta kiwango kikubwa cha amani na utulivu wa kiuchumi tangu achukuwe madaraka mwaka 1986 baada ya kushinda vita vya msituni.
Tangu hapo, mafanikio yake yakawapendeza washirika wa Magharibi, ambao wanaitukuza Uganda kwa kutuma wanajeshi wa kulinda amani kwenye maeneo yenye mizozo mikubwa na migumu kama vile Somalia.
Lakini sasa akiwa na umri wa miaka 71, wafadhili wa mataifa ya Magharibi wanaonekana kuchoshwa na kung'anga'ania kwake madarakani kwa muda mrefu na kwa sauti kubwa wamekuwa wakimtolea wito yeye pamoja na viongozi wengine wa Kiafrika - kama Paul Kagame wa Rwanda - kuachia madaraka ili utamaduni wa kukabidhiana madaraka kwa njia za amani uanzishwe.
Kwenyewe nchini Uganda, wapinzani wa Museveni wanalalamika kwamba mkuu huyo wa waasi aliyegeuka mkuu wa dola anaifanya hazina ya nchi kama kasha lake binafsi katika taifa hilo ambalo bado limeendelea kuwa miongoni mwa masikini kabisa barani Afrika.
Museveni "anaamini kwamba kila mtu ananunulika na anawanunua watu kama vile mifugo sokoni", anasema Amama Mbabazi, mgombea urais na aliyewahi kuwa waziri mkuu na rafiki mkubwa wa Museveni.
Wapinzani walalamikia kuandamwa
Mbabazi na Kizza Besigye, mpinzani wa muda mrefu ambayo amepoteza mara tatu kwenye uchaguzi, ndio washindani wakuu wa Museveni.
Wana ufuasi mkubwa na mikutano yao hukusanya maelfu ya watu kusikiliza namna wawili hao wanakosoa matumizi ya serikali. Mbabazi anaahidi kuyakata matumizi ya ikulu kwa asilimia 60. Wagombea wote wawili wanasema serikali inatumia vyombo vya dola kuwaandama wao na wafuasi wao, madai yanayokanushwa na polisi. Wakati walipowekwa kizuizini mwaka jana, polisi walisema walikuwa wamevunja sheria kwa kufanya kampeni kabla ya muda ulioruhusiwa.
Msemaji wa serikali, Shaban Bantariza, alisema madai kuwa chama cha Museveni kinatumia fedha za walipa kodi kuendeshea kampeni ni "uvumi mtupu." Alisema umangimeza wenye gharama ndio "bei ya demokrasia."
Lakini kwenye bajeti ya mwaka 2015/2016, mwaka wa uchaguzi, matumizi ya serikali yalipanda kwa asilimia 71, na kuifanya sarafu ya nchi hiyo kushuka thamani kwa kiwango ambacho haijawahi kutokea.
"Utawala wake wote umejikita kwenye mfumo wa kugawa fadhila tu," anasema Nicholas Opiyo, mwanasheria kwenye mji mkuu Kampala, maoni ambayo pia yanatajwa na waangalizi wa uchaguzi huo. "Pana mstari mwembamba mno kiasi cha kwamba huwezi kusema ipi ni fedha ya serikali na ni ipi ya chama tawala. Museveni ndiye serikali na serikali ni Museveni nchini Uganda."
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman