Vyama vya Tshisekedi, Kabila vyaanza kuvutana
10 Aprili 2019Mwandishi wa DW mjini Kinshasa anasema chama cha FCC kililezea kuhuzunishwa kwake na matamshi hayo ya Rais Tshisekedi akiwa Washington wiki iliyopita.
Tshisekedi alisema ameomba msaada wa Marekani ili kungo’a mizizi ya udikteta wa serikali iliyopita.
Kwenye taarifa iliyotolewa na chama hicho cha rais wa zamani, Joseph Kabisa, kilisema "matamshi hayo hayatochangia kuweko na mshikamano wa kitaifa kwenye serikali ya mseto."
Chama hicho pia kilikosoa vikali matumizi ya fedha za umma yaliyofanywa na Rais Tshisekedi mnamo kipindi cha miezi miwili tu ya utawala wake.
Wadadisi wa mambo wanasema ushirikiano wa chama cha Tshisekedi na kile cha Kabila hauwezi kudumu daima kutokana na tofauti kubwa za kimiitizamo.
Tshisekedi agoma kumteuwa waziri mkuu wa Kabila
Katika hatua nyengine, duru za kuaminika zinaelezea kwamba Rais Tshisekedi amekataa katakata kumteuwa waziri mkuu aliyependekezwa na Kabila.
Alebert Yuma, ambaye ni mshirika wa karibu wa Kabila, alitakiwa kuteuliwa kuwa waziri mkuu, lakini Tshisekedi hadi sasa bado hajatangaza jina lake.
Duru kutoka ikulu zinaelezea kwamba Tshisekedi ameomba apewe jina jengine, kwani Yuma, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya madini iitwayo GECAMINES, hana sifa nzuri ya uongozi.
Wakati huo huo, uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi Machi, ulifanyika siku ya Jumatano (10 Aprili), huku matokeo yake yakitarajiwa jioni ya siku hiyo.
Uchaguzi huo wa magavana ulijumuisha majimbo 24 miongoni mwa 26 ya Kongo, huku ule majimbo mawili ya Kivu ya Kaskazini na na Maindombe uchaguzi ukiahirishwa hadi Mei 30.
Katiba ya Kongo inaelezea kwamba ni wabunge wa majimbo ndio wanaochaguwa maseneta pamoja na magavana wa majimbo.
Awali, tuhuma za rushwa zilipelekea uchaguzi huo wa magavana kuahirishwa mwezi Machi na kusababisha maandamano ya wafuasi wa chama tawala cha UDPS kufuatia matokeo ya uchaguzi wa maseneta.
Imetayarishwa na Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa