1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya siasa kujadili hali ya usalama

Salma Said25 Oktoba 2015

Baraza la vyama vya siasa nchini Tanzania limekutana visiwani Zanzibar kutafakari mwenendo wa kampeni za wagombea uongozi katika ngazi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais kwa uchaguzi wa Oktoba 25.

https://p.dw.com/p/1Go47
Picha: Imago

Kikao hicho kilichoandaliwa na ofisi ya mrajisi wa vyama vya siasa Tanzania kiliwashirikisha wajumbe wa baraza hilo ambao washiriki wake ni vyama 22 vya siasa vilivyopo Tanzania huku wageni waalikwa wakiwa ni Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na jeshi la polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray wa Chama cha PPT-Maendeleo, alisema jeshi la polisi limeahidi kufanya kazi zake kwa uweledi, katika wakati huu ambapo joto la uchaguzi linazidi kupanda.

Pamoja na suala la ulinzi na usalama katika uchaguzi mkuu huo, mada nyengine iliyowasilishwa katika kikao hicho ni usimamizi na utekelezaji wa wa maadili ya vyama vya siasa, ambapo mwenyekiti huyo alisema baada ya majadiliano "pande zote husika zimevirai vyama kuzungumza na kuwanasihi wafuasi wao kutii sheria za nchi bila ya shuruti."

Miongoni mwa masuala yanayozuwa utata mkubwa kwenye uchaguzi huu ni tangazo la vyama vya upinzani kuwataka wafuasi wao kukaa umbali wa mita 200 baada ya kupiga kura zao kwa kile kinachosemwa kuwa ni "kulinda kura zisiibiwe." Hata hivyo, Mziray alisema wamekubaliana kwamba baada ya kura kuhesabiwa wananchi wanaweza kuyapiga picha na kuangalia matokeo vituoni, huku akisisitiza kuwa "chama cha siasa kitakachosema kimeibiwa kura basi lazima kwanza kiwe na ushahidi wa kutosha.".

Katika hatua nyengine baraza hilo limewaomba waandishi wa habari wasaidie jamii kuwaelimisha katika kuachana na propaganda za mitaani, lakini jeshi la polisi lilijikuta kwenye wakati mgumu kwa malalamiko ya kuvishirikisha vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kazi zao, kinyume na sheria za uchaguzi.

Mwandishi: Salm Said
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman