1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya siasa kali vyahofiwa kuongeza viti Bunge la Ulaya

26 Mei 2019

Wakati matokeo rasmi ya uchaguzi wa Bunge la Ulaya yakisubiriwa hivi leo, pande zote mbili za vyama vinavyopinga Umoja wa Ulaya na vile vinavyouunga mkono zinatarajia kuongeza viti vyao bungeni.

https://p.dw.com/p/3J6c0
Symbolbild | Europawahlen 2019
Picha: picture-alliance/dpa/PA Wire/R. Brown

Uchaguzi huu ambao unahitimishwa leo kwa mataifa 21 kati ya 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya kupiga kura zao, ulitandwa tangu awali na mzozo wa Uingereza kujiondowa kwenye Umoja huo, huku chama cha kihafidhina kikishindwa vibaya. 

Daniel Hannan, mbunge wa Bunge la Ulaya kutokea chama hicho cha Conservative, alisema alikuwa akihofia kuwa chama chake kinakabiliwa na hatari ya kufutwa kabisa na kwamba kingeshindwa kupata kiti hata kimoja kati ya viti 73 vya Uingereza kwenye Bunge hilo.

Chama hicho cha kihafidhina kilionekana kuadhibiwa kwa kushindwa kuitoa nchi hiyo kutoka Umoja wa Ulaya kama kilivyokuwa kimeahidi. 

Maoni ya wapigakura yalionesha kuwa chama kipya kiitwacho Brexit kinachoongozwa na Nigel Farage kilikuwa na nafasi ya kuchukuwa kura nyingi zaidi. 

Kulihofiwa pia kuwa chama kinachofuata siasa za wastani cha Liberal Democrat na ambacho kinataka kuzuwia Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya nacho kingelipata pigo kwenye uchaguzi huu. 

Kwenye uchaguzi wa mwisho wa Bunge la Ulaya mwaka 2014, chama cha Farage cha UKIP kilipata asilimia 27 ya kura, hali ambayo ilisaidia sana kujenga mazingira ya Uingereza kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya miaka mitatu baadaye.

Wacatalan wawapigia kura viongozi walio jela

Symbolbild | Europawahlen 2019
Picha: Getty Images/AFP/N. Hallen

Raia wa Uhispania kwenye jimbo la kaskazini mashariki la Catalonia walipiga kura kwenye uchaguzi huo, huku miongoni mwa wagombea wakiwemo viongozi wa ngazi za juu ambao waliwania wakiwa jela na au uhamishoni.

Rais wa zamani wa jimbo hilo, Carles Puigdemont, na naibu wake wa zamani, Oriol Junqueras, walikuwa miongoni mwa wagombea hao. Ambapo Jungueras yuko jela ya Madrid akingojea hukumu ya mashitaka dhidi yake yanayojumuisha uasi kwa kushiriki kwake kwenye jaribio la Catalonia kutaka kujitenga na Uhispania mwaka 2017, mwenzake Puigdemont anatakiwa nchini kwake kukabiliana na mashitaka kama hayo na amekimbilia Ubelgiji.

Wote wawili wameruhusiwa kuwania kwenye uchaguzi huu, ingawa watakabiliwa na vikwazo vya kisheria endapo watachaguliwa kuwa wajumbe wa Bunge la Ulaya.

Uchunguzi wa maoni kuelekea uchaguzi huu ulionesha kuwa wakaazi wa jimbo hilo tajiri wamegawanyika kuhusiana na suala la kujitenga. Suala hili si maarufu kwenye maeneo mengine ya Uhispania. 

"Nadhani kuna mengi yako hatarini kwa Catalonia panapohusika uchaguzi wa Ulaya," alisema mfanyabiashara Manuel Guajardo, baada ya kupiga kura yake mjini Barcelona, mji kuu wa jimbo hilo. "Kura hii itakuwa ni tafsiri ya watu kufuata muelekeo mmoja ama mwengine, na uchaguzi huu utaashiria hilo."

Ufaransa na Ujerumani zapiga kura

Symbolbild | Europawahlen 2019
Picha: Getty Images/AFP/G. Kirk

Raia nchini Ufaransa na Ujerumani, mataifa yenye nguvu na ushawishi mkubwa barani Ulaya, nao walipiga kura katika siku ya mwisho ya uchaguzi, huku vyama vinavyopinga Umoja wa Ulaya na uhamiaji vikitumai kutoa changamoto kubwa. 

Nchini Ujerumani, maoni ya umma ya kabla ya uchaguzi yalivipa nafasi ya ushindi wa asilimia 28 vyama ndugu vya kihafidhina vya CDU na CSU. 

Wanasiasa kutoka vyama vikuu nchini Ujerumani walitumia siku za mwisho kabla ya uchaguzi kutoa onyo dhidi ya kukipigia kura chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kinachopinga wahamiaji na Umoja wa Ulaya.

Mbali ya Ujerumani na Ufaransa, nchi nyingine karibu 20 wanachama wa Umoja huo zilipiga kura katika siku ya mwisho ya uchaguzi huo wa Bunge la Ulaya. 

Zaidi ya wapiga kura milioni 400 walishiriki uchaguzi huo katika mataifa 28 na matokeo rasmi yalitarajiwa baadaye jioni ya Jumapili (26 Mei). 

AP