Vyama vinavyounga mkono kujitenga Catalonia vyashinda
22 Desemba 2017Wafuasi wa aliyekuwa kiongozi wa jimbo hilo Carles Puigdemont walisikika wakishangilia wakati matokeo ya uchaguzi huo yalipotangazwa hapo jana usiku na kusema Puigdemont ni rais wao.
Chama cha Puigdemont cha mrengo wa kushoto cha ERC na kile kinachopinga ubepari cha CUP vyote kwa pamoja vimeshinda viti 70 kati ya viti 135 vya bunge la jimbo hilo licha ya kupata asilimia 47.5 ya kura. Vyama hivyo bado vitahitaji kukubaliana ili kuunganisha nguvu kuunda serikali lakini kwa sasa wafuasi wa vyama hivyo kwa pamoja wanasherehekea matokeo ya ushindi huo mzito ambao unakaribia kuwa kama ule wa mwaka 2015.
Mmmoja waakazi wa jimbo hilo la Catalonia Francesc Portella alisikika akisema matokeo hayo ni salamu tosha kwa serikali ya Uhispania na ulaya kwa ujumla kuwa kuna haja sasa ya kukaa pamoja na kujadili juu ya mustakabali wa kisiasa wa nchi hiyo.
Uchaguzi huo umefanyika huku Carles Puigdemont akiwa nchini Ubeligiji ambako alikimbilia baada ya kutangaza uhuru wa jimbo hilo mnamo Oktoba 27 hatua ambayo ilikataliwa na serikali ya mjini Madrid na kuchukua madaraka ya moja kwa moja ya jimbo hilo lililokuwa na utawala wa ndani na hatimaye kutangaza kuitisha uchaguzi wa mapema.
Puigdemont asema wacatalonia wameshinda
Akizungumza akiwa uhamishoni mjini Brussels Carles Puigdemont ameita matokeo ya uchaguzi huo kuwa ni ushindi kwa watu wa Catalonia na kusisitiza kuwa ushindi huo ni sawa na kofi la uso kwa waziri mkuu wa Uhispania Mariaono Rajoy.
Ameongeza kuwa kwa mtizamo wake anaona wameshinda na wana haki sasa ya kusikilizwa.
Makamu wa rais wa bunge la Catalonia Agust Alcobero alitangaza ushindi huo kwa niaba ya wale wanaounga mkono kujitenga na kusema wanaotaka kujitenga wameshinda na kutoa mwito kuachiwa huru kwa wanasiasa wa jimbo hilo walioko jela pamoja na kurejeshwa madarakani iliyokuwa serikali ya jimbo hilo.
Matokeo ya uchaguzi huo yanaonekana pia kuwa pigo kubwa dhidi ya waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy ambaye alikuwa na matumaini kuwa uchaguzi huo utazima kabisa ndoto za jimbo la Catalonia kutaka kujitenga.
Aidha matokeo haya yanaashiria kwa kiasi fulani kuendelea kuchochea mgogoro wa kisiasa nchini Uhispania.
Makamu wa waziri mkuu wa Uhispania mwishoni mwawiki alidai kuwa chama tawala nchini humo cha Popula Party (PP) kimezima kabisa vuguvugu linalouunga mkono kujitenga kwa jimbo la Catalonia kufuatia aliyekuwa kiongozi wa serikali ya jimbo hilo Carles Puigdemont kuwa uhamishoni nchini Ubeligiji huku makamu wake Oriol Junqueras akiwa jela.
Uchaguzi huo wa mapema uliofanyika jana Alhamisi uliaamuriwa na waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy baada ya jimbo hilo kutangaza kujitenga kufuatia kura ya maoni ya Oktoba mosi ambayo mahakama ya Uhispania ilisema ni kinyume cha katiba.
Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE/DW
Mhariri :Yusuf Saumu