"Vyama vina hisia mbaya juu ya NEC na ZEC"
27 Oktoba 2015Katika tamko lao la awali mbele ya waandishi wa habari waangalizi hao wamesema kuwa uchaguzi wa mara hii ulikuwa na ushindani mkali huku kukishuhudiwa idadi kubwa ya watu wakijitokeza kupiga kura katika hali ya utulivu na amani.Waangalizi hao wamesema kuwa pamoja na kwamba tume hizo zilijiandaa vyema kufanikisha uchaguzi huo lakini kutokuwepo kwa dhana ya uwazi na kukosekana kwa maelezo muafaka kuhusu daftari la kudumu la wapiga kura kumesababisha kujitokeza kwa hisia mbaya kwa vyama vya siasa juu ya tume hiyo. Waangalizi hao wamesema kuwa mambo hayo kumesababisha pia kwa vyama vya siasa kupoteza imani juu ya mchakato huo wa uchaguzi.
Akisoma tamko hilo, Mwangalizi Mkuu wa Umoja huo wa Ulaya, Judith Sargentini, alisema kuwa alikaribisha namna ushindani mkubwa uliojitokeza kwenye uchaguzi wa safari hii, lakini akasisitiza kuwa tamko hilo ni la awali kwa vile bado shughuli za uchaguzi zinaendelea. “Napenda kusisitiza hili kwamba, taarifa hii inatolewa wakati ambapo kazi ya kujumlisha matokeo ingali ikiendelea, hivyo ifahamike kwamba taarifa hii siyo tamko la mwisho kuhusiana na tathmini ya waangalizi wa Umoja wa Ulaya," alisema Sargentini. "Tunavyozungumza waangalizi wetu wanaendelea kufuatilia zoezi la ujumlishaji wa matokeo.”
Umoja wa Ulaya ni sehemu ya waangalizi wa kimataifa walioko nchini kwa ajili ya kufuatilia uchaguzi huu ambao pia umeshuhudia baadhi ya vigogo wa kisiasa wakiangushwa kwenye majimbo yao. Waangalizi wengine ni pamoja na Umoja wa Afrika na wale kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC. Ama waangalizi hao wa Ulaya wamesema wataendelea kusalia nchini hadi hapo Novemba 15, katika kipindi hicho itajihusisha na majukumu kadhaa ikiwamo kukutana na vyama vya siasa, maofisa wa uchaguzi wa asasi za kiraia. Umoja huo umetuma jumla ya waangalizi 141 waliosambazwa katika vituo vyote 625 vya upigaji wa kura. Huu ni ujumbe mkubwa zaidi kuwahi kutumwa na umoja huo kufuatilia uchaguzi wa Tanzania.