1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Picha 7
14 Februari 2017
https://p.dw.com/p/2XYSl

Mimea ya mahindi Afrika Kusini na Zimbabwe inakabiliwa na hatari ya viwavi jeshi. Ni tatizo ambalo limekuwa changamoto kwa wakulima Amerika kaskazini na kusini, lakini uwepo wake Afrika ulirekodiwa mwaka mmoja uliopita Sao Tome na Principe.

Kituo cha kimataifa cha ukulima na sayansi (CABI), kilicho na afisi nyingi kote duniani, kimeonya kwamba mdudu huyo anayeishi kwa kula mimea kama mahindi, anaweza kuenea hadi Asia na Mediterenia, na kuzua tisho kwa biashara ya kilimo kote ulimwenguni.

Godfrey Chikwenhere kutoka kwa wizara ya kilimo ya Zimbabwe aliliambia shirika la habari la dpa kwamba mdudu huyo mdogo, aliyeonekana nchini humo mara ya kwanza Desemba mwaka jana, alikuwa  kufikia katikati ya mwezi uliopita ameshasamba katika mikoa yote. Ingawa alisema kwamba mazao yalioathirika zaidi yalikuwa ni mahindi, alisema kupungua kwa mazao kumekuwa kwa kiasi kidogo.

"Tungali tu katika harakati za kumdhibiti mdudu huyu," alisema. "Tumetuma kikosi cha watu wakanyunyize dawa katika maeneo yayliyoathirika."

Afrika Kusini inasema pia kwamba imebuni mpango wa dharura wa kukabiliana na mdudu huyo, ikiwemo kampeni ya uhamasishaji na majaribio ya dawa za kuwakabili.

Inaaminika kiwavi jeshi huyu alifika  Afrika kwa kuwemo ndani ya ndege.