Viwanja: Kombe la Dunia Urusi 2018
Kombe la Dunia Urusi litachezwa katika viwanja 12 kati ya mwezi Juni 14 na Julai 15. Ifuatayo ni orodha ya viwanja vitakavyotumika kwenye kundumbwendumbwe hicho.
Uwanja wa Luzhniki, Moscow
Uwanja mkuu, ambao utatumiwa na timu ya taifa ya Urusi, una uwezo wa kupokea mashabiki 81,000. Ndipo mechi ya ufunguzi na ya fainali la Kombe la Dunia zitakapochezwa, na vile vile mechi ya nusu fainali. Uwanja huu ambao umekarabatiwa kwa sababu ya Kombe la Dunia umewahi kutumiwa kwa mashindano ya fainali ya ligi ya washindi na Michezo ya Olimpiki wakati wa majira ya joto.
Yekaterinburg Arena
Uwanja wa Yekateringburg Arena, uliojengwa mwaka 1953 umekarabatiwa kwa sababu ya Kombe la Dunia mwaka 2018. Uwanja huu wenye uwezo wa kupokea mashabiki 35,000, ni uwanja wa nyumbani wa timu ya FC Ural katika divisheni ya kwanza ya Urusi. Yekaterinburg ndio iliyo mashariki zaidi ya miji yote iliyoandaa kombe hilo.
Uwanja wa Saint Petersburg
Uwanja mpya wa nyumbani wa timu ya Zenit St. Petersburg una uwezo wa kukaliwa na mashabiki 68,000. Katika uwanja huu itachezwa mechi moja ya nusu fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu. Aidha utatumiwa kuandaa michezo kwenye makundi, ukiwemo ule ambao Urusi itashiriki. Uwanja wa Saint Petersburg ulitumika kuandaa michezo ya kombe la Masharikisho mwaka 2017.
Samara Arena
Uwanja huu wenye uwezo wa kukaliwa na mashabiki 44,000 ulijengwa kwa sababu ya Kombe la Dunia katika kisiwa kilichoko kusini mwa Samara mahali ambapo hapakuwa na miundombinu. Hapa ndipo wenyeji Urusi watakapocheza mechi yao ya mwisho ya makundi. Robo fainali pia itachezwa hapa, utakuwa uwanja wa nyumbani wa timu ya Krylya Sovetov, ambayo sasa iko katika divisheni ya pili.
Volgograd Arena
Uwanja huu ulijengwa katika uliokuwa uwanja mkongwe wa eneo la Volgograd karibu na mto Volga. Una uwezo wa kuwapokea mashabiki 45,000 na utatumika tu kwenye mechi za makundi. Baada ya michuano ya kombe la dunia utakuwa uwanja wa nyumbani wa timu ya Rotor Volgograd, inayocheza katika ligi ya divisheni ya pili. Volgograd ilikuwa inafahamika kama Stalingrad.
Mordovia Arena, Saransk
Msarifu majengo wa Ujerumani Tim Hupe alichora muundo wa uwanja huu kwa sababu ya kombe la dunia. Una uwezo wa kukaliwa na mashabiki 44,000 na utatumiwa kwa ajili ya mechi za makundi pekee. Baada ya michuano ya kombe la Dunia, utakabidhiwa timu ya Mordovia Saransk inayocheza katika ligi ya divisheni ya tatu.
Rostov Arena
Uwanja wa Rostov una uwezo wa kuwachukua mashabiki 45,000 ni moja ya viwanja vipya vilivyojengwa kwa sababu ya Kombe la Dunia. Uwanja huu utatumiwa kuandaa mechi ya makundi na mechi moja ya mwisho ya timu 16. Utakuwa uwanja mpya wa nyumbani wa timu ya FC Rostov baada ya michuana hii.
Uwanja wa Nizhny Novgorod
Uwanja huu wenye uwezo wa kukaliwa na mashabiki 45,000 ulijengwa maalum kwa Kombe la Dunia. Utatumiwa kuandaa mechi nne za makundi pamoja na robo fainali. Baada ya michuano unatarajiwa kuwa uwanja wa nyumbani wa timu ya Olimpiyets Nizhny Novgorod ya ligi ya divisheni ya pili, isipokuwa mwezi Machi 2017, aliyekuwa gavana Valery Shantsev alisema utatumika pia kwa michezo mingine.
Uwanja wa Kaliningrad
Huu ndio uwanja pekee unaoandaa Kombe la Dunia nje ya Urusi — Kaliningrad ni himaya kati ya Poland na Lithuania. Uwanja huu wenye uwezo wa kupokea mashabiki 35,000-ulijengwa hususan kwa Kombe la Dunia. Uwanja huu utatumika kwa sababu ya mechi za makundi na utakuwa uwanja wa mpya wa nyumbani wa Baltika Kaliningrad, timu iliyoko kwenye divisheni ya pili.
Uwanja wa Spartak, Moscow
Ijapokuwa ulitumika kwenye kombe la Mashirikisho, uwanja wa Spartak wenye uwezo wa kukaliwa na mashabiki 45,000, utatumiwa tu kuandaa mechi za makundi na mechi za mtoano. Uwanja huu ulifunguliwa tena mwaka 2014, ni uwanja wa nyumbani wa timu ya Spartak Moscow, timu maarufu nchini Urusi.
Kazan Arena
Uwanja huu ulitumika kwenye mechi za Kombe la Mashirikisho, uwanja wa Kazan utatumika kuandaa mechi za mwisho za timu 16, robo fainali na mechi nne za makundi. Uwanja huu una uwezo wa kukaliwa na mashabiki 41,585. Rais wa Urusi Vladimir Putin aliweka jiwe la msingi kabla ufunguliwe mwaka 2013. Ni uwanja wa nyumbani wa Rubin Kazan.
Uwanja wa Fisht, Sochi
Uwanja huu una nafasi kwa mashabiki 41,220 na ulijengwa kwa sababu ya michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi iliyoandaliwa mwaka 2014. Sehemu kubwa ya paa imeondolewa kwa sababu ya kandanda. Mchuano wa mwisho pamoja na robo fainali zitachezwa hapa pamoja na mechi nne za makundi.