1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viva Espana! Uhispania yaingia fainali ya kombe la dunia

Josephat Nyiro Charo8 Julai 2010

Hispania nzima imegeuka kuwa uwanja wa shangwe na nderemo kufuatia ushindi wa timu yao wa bao 1:0 dhidi ya Ujerumani kwenye ngoma ya nusu fainali iliyochezwa jana katika uwanja wa mjini Durban Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/ODjQ
Mchezaji wa Ujerumani, Bastian Schweinsteiger, kushoto, na Sergio Ramos wa Hispania waking´ang´nia mpira huku Xavi Hernandez, kulia, akiwatazamaPicha: AP

Bao la Carles Puyol alilolifunga kwa kichwa katika dakika ya 73 baada ya kona, lilitosha kuyazika matumaini ya Wajerumani kuingia katika fainali ya kombe la dunia.

Hispania sasa itamenyana na Uholanzi kwenye fainali kwa mara ya kwanza katika historia, Jumapili ijayo Julai 11 katika uwanja wa Soccer City mjini Johannesburg. Wajerumani wanasubiri kuvaana na Uruguay kwenye ngoma ya kuwania nafasi ya tatu Jumamosi ijayo Julai 10 katika uwanja wa Port Elizabeth.

Ni tukio la kihistoria. Tumeingia fainali ya kombe la dunia. Hiyo si ndoto tena! Hizo ndizo hisia zilizojitokeza nchini Hispania kufuatia ushindi huo. Maelfu na maelfu ya mashabiki wameimba na kupeperusha bendera za Hispania nje ya uwanja wa Bernabeu mjini Madrid ambako mechi kati ya Ujerumani na Hispania ilionyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni kubwa.

"Uhispania ilidhibiti mchezo na ilikuwa na nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao kuliko Ujerumani. Na katika kipindi cha pili Wajerumani walionekana tayari ni kana kwamba wamechoka", amesema Tomas Vasquez, shabiki aliyeuangalia mpambano huo pamoja na mwanawe katika uwanja wa Bernabeu.

Karibu kila mji nchini kote Uhispania kuliwekwa televisheni kubwa kuwawezesha watu kutizama mechi hiyo, lakini mjini Barcelona, mji mkuu wa jimbo la Catalonia, mambo yalikuwa tofauti ingawa wachezaji saba wa kikosi cha Uhispania kilichoingia uwanjani dhidi ya Ujerumani, wanatokea timu ya Barcelona.

Kocha wa Ujerumani Joachim Löw amesema wamehuzunika na kuvunjwa moyo, lakini Uhispania imeonyesha mchezo mzuri. Ameipongeza Uhispania akisema imekuwa ikicheza vizuri kwa miaka miwili au mitatu iliyopita.

Jogi Löw Blauer Pulli
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew, kushoto, na naibu wake Hans-Dieter FlickPicha: picture-alliance/dpa

Naye nahodha wa timu ya Ujerumani, Philip Lamm amesema, "Nadhani tungeweza leo kuishinda Uhispania. Timu yetu imecheza vizuri sana kwenye mashindano haya, lakini inauma sana kutolewa kwenye nusufainali."

Mlinda lango wa Ujerumani, Manuel Neuer amekiri hawakucheza vizuri, "Hatukucheza sana kwenda mbele na tumefaulu kutengeneza nafasi chache mno za kufunga. Uhispania ilikuwa na nafasi nyingi zaidi na sisi leo tumekosa ushujaa kidogo."

Wajerumani wamejitahidi kutotokwa na machozi huku kimya kikitanda nchi nzima kufuatia timu yao kushindwa na Uhispania. Mamilioni ya Wajerumani walibakia vinywa wazi wakishuhudia timu yao ya kandanda, ikitolewa jasho na Wahispania na hatimaye kufungwa bao 1:0 kama ilivyoshindwa wakati wa fainali ya kuwania kombe la Ulaya mnamo mwaka 2008 ambapo ilishindwa kwa bao 1:0.

Kwa Ujerumani ambayo imemiminiwa sifa kubwa kwa kiwango cha mchezo iliyoonyesha kwenye michuano ya kuwania kombe la dunia Afrika Kusini, kushindwa na Hispania kumesababisha uchungu usio mithili miongoni mwa washabiki wa soka humu nchini. "Nahisi ni kama matanga, ni huzuni kubwa, moyo wangu unaniuma," amesema Lucia Perschke, shabiki wa umri wa miaka 38, aliyeutizama mchuano wa nusu fainali pamoja na marafiki mjini Berlin.

Huko mjini Hamburg, kulikuwa na kimya chenye mshindo mkubwa, huku mashabiki wakionekana wakitembea kwa miguu na wengine wakipeleka baiskeli zao kurejea nyumbani. Sauti ya vuvuzela moja tu ndiyo iliyosikika mjini humo. Msichana mdogo wa miaka saba akilia kwa uchungu huku machozi yakimtiririka saa nzima baada ya kipenga cha mwisho kulia katika uwanja wa Durban, kulikochezwa ngoma hiyo kati ya Ujerumani na Hispania.

NO FLASH Fußball WM 2010 Südafrika Halbfinale Deutschland Spanien
Timu ya UjerumaniPicha: AP

Yote yamekwisha! Limeandika gazeti la Bild la hapa Ujerumani kwenye tovuti yake na kuongeza kwamba mechi ya kuwania nafasi ya tatu, kama ilivyokuwa wakati wa mashindano ya kombe la dunia mwaka 2006 hapa Ujerumani, si mchuano wa kufutia machozi. Mashabiki wamevunjika moyo. Machozi yanatirika kwenye maeneo yaliyotengwa kutizama mechi za kombe la dunia nchini kote. Lakini hata kama inauma, Hispania ilistahili kushinda, limeendelea kuandika gazeti la Bild.

Ingawa mashabiki wengi walikwenda nyumbani kimya kimya, kunao baadhi ambao walijawa na hasira na kuzusha vurugu huko mjini Berlin na hivyo kukabiliana na polisi. Wajerumani wanalazimika kusubiri matokeo ya mechi kati ya timu yao na Uruguay Jumamosi ijayo kuwa na nafasi nyengine tena ya kusherehekea na kupuliza mavuvuzela!

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman