Vituo vya kuwahifadhi wahamiaji si jibu sahihi kwa EU
4 Julai 2018Hayo yamesemwa na shirika la uhamiaji la Umoja wa mataifa kuhusiana na wazo ambalo shirika hilo limeombwa kulitekeleza.
Wahamiaji kuvuka bahari na kuingia katika mataifa ya Ulaya wamepungua kwa kiasi kikubwa, na ni kiasi ya watu 45,000 tu ambao wamefanikiwa kuingia Ulaya mwaka huu. Lakini suala hilo nyeti kabisa linapeleka mbio ajenda ya kisiasa ya Umoja wa Ulaya.
Wiki iliyopita, mataifa ya Umoja wa Ulaya yalikubaliana kubana mipaka yao ya nje na kutumia fedha zaidi katika mataifa ya Mashariki ya kati na Afrika kaskazini kupunguza idadi ya wanaowasili katika mipaka yao.
Kansela Angela Merkel , akijaribu kuokoa muungano wake unaounda serikali , siku ya Jumatatu alikubali kuunda makambi ya wahamiaji katika mipaka ya Ujerumani, ikionesha jinsi gani Umoja wa Ulaya unashindwa kukubaliana kuhusu sera ya pamoja ya uhamiaji na serikali mbali mbali zikizidi kuchukua hatua za binafsi.
Kitu kimoja viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana ni kuangalia jinsi ya kujenga vituo vya kufikia ili kuwahifadhi wale waliookolewa kutoka katika safari yenye hatari ya kuvuka bahari ya Mediterania. Wengi wanafika ufukweni nchini Italia, lakini zaidi ya watu 1,300 wamefariki mwaka huu.
"Bahari ya Mediterania ni eneo linalohusika na nchi nyingi, kaskazini hadi kusini. Tuna jukumu la pamoja kuongoza kile kinachotokea katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuepuka watu kufa maji," Euginio Ambrosi , mkuu wa shirika la kimataifa kwa ajili ya wahamiaji, IOM , ujumbe wa Umoja wa Ulaya aliliambia shirika la habari la Reuters.
Vipo vituo 10 vya kuwahifadhi wahamiaji
Shirika la IOM pamoja na lile la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR, yanatakiwa kusaidia katika kuendesha vituo hivyo.
Ambrosi amesema vituo 10 vilivyopo hivi sasa vya kuwahudumia wahamiaji nchini Ugiriki na Italia vinawezekana kuimarishwa na vingine vipya vinaweza kuongezwa nchini Malta. Lakini kufungua vipya katika eneo hilo la kusini la bahari ya Mediterania , kama baadhi ya mataifa ya Umoja wa ulaya yanavyotaka, vitachukua muda.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani tayari inafanyakazi kutayarisha makubaliano pamoja na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya kuwarejesha wakimbizi nchini ambazo walijiandikisha kwanza , kuomba hifadhi, msemaji wa wizara hiyo amesema leo.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer anatarajiwa kwenda Vienna leo, ambako atakutana na kansela wa Austria Sebastian kurz, pamoja na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban anatarajiwa kukutana na kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin.
Wakati huo huo, makundi ya kutoa misaada yamesema mfumo wa Ufaransa wa kuwahudumia idadi kubwa ya watoto wahamiaji ambao hawana wazazi hauna mpango maalum na unawadhuru wale ambao wanahitaji msaada. Ripoti iliyotolewa leo , na shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch lilieleza mfumo huo wenye mkanganyiko kwamba unakandamiza watoto.
Kundi la kutoa misaada la madaktari wasio na mipaka walisisitiza taarifa hiyo kwa kusema kushindwa kwa Ufaransa ni kutokana na kufikiria kwamba mtu anayedai kwamba yuko chini ya miaka 18 anadanganya. Watu kiasi ya 25,000 vijana wanaodai hawana watu waliofuatana nao ambao ni watoto wahamiaji waliwasili nchini humo mwaka jana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape
Mhariri: Idd Ssessanga