Vituo vya jeshi la Marekani na Ulaya vyashambuliwa Somalia
30 Septemba 2019Kundi la waasi wa itikadi kali nchini Somalia wamefanya mashambulizi mawili dhidi ya vituo vya wanajeshi wa Marekani na Ulaya. Shambulio la kwanza lilifanywa dhidi ya eneo la kurushia ndege ambalo ni kambi ya wanajeshi wa Marekani na Somalia katika mkoa wa Lower Shebelle kusini mwa Somalia. Kwa mujibu wa afisa usalama, wa mkoa wa Lower Shebele ,Yusuf Abdourahman, mshambuliaji wa kujitoa muhanga ndani ya gari aliliripua gari lilokuwa limesheheni mabomu mbele ya geti la eneo la kurusha ndege la Belidogle. Milio ya risasi ilisikika kwenye eneo zima la kambi hiyo baada ya mashambulio hayo, kuonesha mashambulizi bado yanaendelea katika kambi hiyo. Kundi la itikadi kali la alshabab limedai kuhusika na shambulio hilo. Wanajeshi wa Marekani hutumia uwanja wa kurushia ndege wa kambi ya Belidogle kurusha ndege zao zisiendeshwa na rubani ambazo zinavishambulia vituo vya al Shabaab na katika shughuli za kutowa mafunzo kwa wanajeshi wa Somalia.