1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyanukia baina ya Ethiopia na Eritrea

Josephat Charo5 Novemba 2007

Ethiopia na Eritrea, mahasimu wakubwa katika pembe ya Afrika, huenda zikaingia vitani kwa sababu ya mzozo kuhusu mpaka katika wiki chache zijazo ikiwa hakuna hatua zozote kubwa zitakazochukuliwa na jumuiya ya kimatiafa kuzizuia. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la kimatiafa linaloshughulikia mizozo, International Crisis Group, ICG.

https://p.dw.com/p/C7fH
Wanajeshi wa Ethiopia
Wanajeshi wa EthiopiaPicha: AP

Watu 70,000 waliuwawa katika vita vya kati ya mwaka wa 1998 na 2000 kati ya Ethioipia na Eritrea na kusababisha matatizo yasiyoweza kuelezeka katika nchi hizo mbili ambazo zimetajwa kuwa maskini zaidi duniani. Sasa wachambuzi wanaonya kwamba huenda hali hiyo ikatokea tena huku wanajeshi wakiendelea kukusanyika katika eneo la mpakani kabla muda uliopewa tume huru ya Ethiopia na Eritrea kuweka mpaka kati ya nchi hizo ukikaribia kumalizika mwishoni mwezi Disemba mwaka huu.

Katika ripoti yake kuhusu mgogoro baina ya Ethiopia na Eritrea shirika la kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG, limesema ukweli kwamba Ethiopia na Eritrea huenda zikaingia vitani ni dhahiri. Ripoti hiyo imesema ongezeko la wanajeshi katika eneo la mpaka wa pamoja kati ya nchi hizo mbili limefikia kiwango cha kutisha na hakutakuwa na suluhisho la kijeshi litakalopatikana kiurahisi ikiwa vita vitazuka tena. Kitakachotokea ni mapigano katika ardhi ya Eritrea, kusambaratika kwa uthabiti wa Ethiopia na kutokea ghafla kwa mzozo mkubwa wa kibinadamu.

Shirika la ICG limeitaka Marekani na Umoja wa Mataifa kutumia uwezo wao kuzidhihirishia Ethiopia na Eritrea kuwa hatua zozote ambazo zitahatarisha uthabiti wa eneo la pembe ya Afrika hazitavumuliwa. Marekani inaiona Ethiopia kuwa mshirika wake mzuri katika eneo hilo, lakini uhusiano wake na Eritrea umekuwa mbaya mno kiasi kwamba Marekani huenda ikaiorodhesha serikali ya mjini Asmara katika orodha ya wadhamini wa ugaidi kwa kuwasaidia wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia.

Umoja wa Mataifa una kikosi cha wanajeshi 1,700 wa kulinda usalama katika eneo la upana wa kilomita 1,000 linalozitenganisha Ethiopia na Eritrea. Shirika la ICG limesema msimamo wa jumuiya ya kimataifa wa imani potovu huenda usababishe maafa makubwa kwa wakaazi wa eneo la pembe ya Afrika.

Ripoti ya shirika la ICG imetolewa baada ya Eritrea kuishutumu Ethiopia mara tatu katika kipindi cha wiki moja kwamba inaandaa uvamizi. Tuhuma hiyo imepingwa vikali na serikali ya mjini Addis Ababa ikiitaja kuwa upuuzi mtupu.

Shirika la ICG linabashiri kuwa ikiwa vita vitazuka, Ethiopia itataka kuuteka mji mkuu Asmara na bandari ya Assab ili kuipindua serikali ya Eritrea. Ikiwa imekatishwa tamaa na kutokuwepo maendeleo, tume ya mpaka inasema Ethiopia na Eritrea zina muda hadi kufikia mwisho wa mwezi huu kuweka mpaka ardhini la sivyo itaweka mpaka huo kwenye ramani na kuuwacha ubaki hivyo.

Wanadiplomasia wana wasiwasi kwamba tarehe hiyo huenda ikawa kama chombo cha kufyatulia risasi na kuzusha moto mkubwa. Shirika la ICG limezilaumu serikali za mjini Addis Ababa na Asmara huku likiueleza utawala wa Eritrea kuwa mojawapo ya tawala dhalimu zaidi barani Afrika na Ethiopia kuwa nchi isiyo na nia ya kuwa demokrasia ya kweli.