1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Yemen vyaendelea

15 Agosti 2017

Yemen iko katika janga kubwa la kibinaadamu. Baada ya miaka miwili ya mapigano makali, vita hivyo sasa vimeelezwa kuwa vita vilivyosahaulika. Misaada ya haraka inahitajika, hasa chakula na afya.

https://p.dw.com/p/2iHO2
YEMEN-CONFLICT-SANAA-STRIKES
Picha: AFP/Getty Images

Historia ya karibuni ya taifa la Yemen ni historia moja iliyokumbwa na migawanyiko na umwagikaji damu. Hadi mapema miaka ya sitini (1960) taifa hilo liliongozwa kwa mfumo wa ufalme eneo la kaskazini na Waingereza wakaongoza eneo la kusini. Mapinduzi katika maeneo yote yalilitumbukiza taifa hili katika vurugu kwa muda mrefu; ambazo hatimaye ziliuvunja muungano mnamo mwaka wa 1990.

Taifa hilo la mashariki ya kati limekuwa miongoni mwa mataifa maskini katika eneo hilo. Mwaka wa 2015 liliorodheshwa katika nafasi ya 168 kati ya nchi 188 katika faharasa ya maendeleo ya binadamu inayopima makadirio ya umri, elimu na viwango vya maisha.

Kabla ya vita, idadi ya wakazi nchini Yemen ya zaidi ya milioni 20 ilitazamiwa kuongezeka maradufu kufikia mwaka 2035. Ikikabiliwa na ukosefu mkubwa wa ajira, na kutoridhishwa na familia iliyoongoza ya rais wa zamani Ali Abdullah Saleh, taifa hilo lilikuwa tayari kwa mabadiliko wakati vuguvugu la maandamano ya kutaka mageuzi la msimu wa mapukutiko katika nchi za kiarabu lilipotokea Afrika Kaskzini na Mashariki ya kati mnamo mwaka 2011.

Je vita hivi vilianza lini?

Vita vya Yemen vilianza katika kipindi cha miaka kadhaa, vikianzia na vuguvugu la maandamano ya msimu wa mapukutiko mwaka wa 2011. Waandamanaji wanaounga mkono demokrasia walifanya maandamano kama njia ya kumlazimisha rais Ali Abdullah Saleh kumaliza utawala wake wa miaka 33. Alijibu kwa kukubali mabadiliko ya kiuchumi lakini akakataa kujiuzulu.

Ilipofika mwezi Machi mwaka huo taharuki iliyozigubika barabara za mji mkuu Sanaa ilipelekea waandamanaji kufa mikononi mwa wanajeshi. Kamanda mmoja maarufu wa jeshi la Yemen akauunga mkono upinzani, hali iliyotoa nafasi ya kutokea kwa ghasia kali kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kikabila.

Majeruhi wakikimbizwa hospitalini
Majeruhi wakikimbizwa hospitalini Picha: AFP/Getty Images

Kutokana na mkataba ulioafikiwa na jumuiya ya kimataifa, hatimaye taifa la Yemen likashuhudia mabadiliko, ya kukabidhiwa madaraka mwezi Novemba kwa makamu wa rais Abed Rabbo Mansour Hadi, hali iliyotoa nafasi ya kufanyika kwa uchaguzi mnamo mwezi Februari mwaka uliofuata, ambapo Hadi alikuwa mgombea pekee. Juhudi za rais Hadi za kutaka kufanya mageuzi ya katiba na bajeti zilizusha upinzani mkali kutoka kwa waasi wa Houthi wanaotokea eneo la kaskazini.

Nani anapigana na nani?

Makundi kadha wa kadha yanajihusisha katika vita vya Yemen. Hata hivyo vita hivyo viligawanyika katika makundi mawili makubwa, vikosi vinavyoiunga mkono serikali ikiongozwa na rais Hadi na vikosi vinavyoipinga serikali vikiongozwa na waasi wa Houthi ambao wanaungwa mkono na rais wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Wahouthi wanatokea kaskazini mwa Yemen na wanatoka kutoka kundi dogo la waislamu wa madhebu ya Shia linaojulikana kama Zaydis. Hadi msimu wa kiangazi mwaka wa 2015, wanamgambo walifaulu kuingia sehemu kubwa kusini mwa taifa la Yemen. Kwa sasa wanadhibiti mikoa muhimu mikuu kaskazini mwa Yemen. Serikali ya rais Hadi imeishutumu Iran kwa kuingiza silaha kwa njia ya magendo, madai yaliokataliwa na serikali ya mjini Tehran.

Makao makuu ya serikali ya rais Hadi yanapatikana katika mkoa wa Aden na inatambuliwa kimataifa kama serikali ya Yemen. Mnamo mwaka 2015 taifa la Saudi Arabia liliingilia kati na kuunda muungano wa kimataifa kama njia ya kumrudisha tena rais Hadi.

Katika miezi ya karibuni, mvutano umejitokeza ndani ya serikali ya Hadi iliyo uhamishoni huku aliyekuwa mshauri wake wa maswala ya usalama, Aidarous al Zubaidi na aliyekuwa waziri Hani Bin Braik wakiongoza vuguvugu la kujitenga wakiungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mwandishi: Fathiya Omar/DW

Mhariri:Josephat Charo