Vita vya maneno vyaendelea kati ya Ethiopia na Eritrea.
6 Machi 2007Katika tukio la karibuni, Ethiopia imedai kwamba ni Eritrea iliohusika na utekaji nyara wa watalii wa kigeni kaskazini mwa Ethiopia. Kwa mtazamo wa baadhi ya wadadisi, nchi hizo mbili zinakabiliwa na kitisho cha kuingia tena vitani.
Eritrea imekua ikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binaadamu , ukiandamana na kutiwa watu ndani, ugaidi unaodhaminiwa na dola na kuteswa wanaokosoa utawala wa nchi hiyo. Mbali na hayo, taifa hilo dogo la pembe ya Afrika lilishutumiwa na jirani yake Ethiopia hivi karibuni katika kile kilichoelezwa kuwa lilikua na mpango wa shambulio la bomu wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa Afrika mjini Addis Ababa- mkutano wa nane uliohudhuriwa na katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki –moon, Viongozi wa Afrika na waakilishi wa umoja wa nchi za kiarabu na umoja wa Ulaya.
Na sasa Eritrea inaadaiwa tena kwamba imehusika na kutekwa nyara watalii watano wakiingereza waliotekwa nyara pamoja na waethiopia mapema juma hili. Tangu wakati huo waethiopia watano wameachiwa huru na mmoja wao kudai kwamba walihusika walikua Waeritrea. Ama Eritrea binafsi inayapinga madai yote hayo na kushambulia vikali Ethiopia kwa kile ilichokiita”Ukahaba wa kisiasa .”
Vita hivi vya maneno vimekuja bila ya kukumbuka maafa ya vita vya kuwania eneo la mpaka kati ya nchi hizo mbili 1998 hadi 2000 ambapo karibu watu 70,000 walipoteza maisha yao- huku wengine wakiviita vita vikuu vya Afrika. Uhasama pia una pamba moto kutokana na uungaji mkono unaofanywa na kila upande kwa makundi yanayoupinga upande wa pili.
Ethiopia inakiunga mkono chama cha Eritrea Democratic Alliance, muungano wa vyama 13 vya upinzani dhidi ya serikali ya kimabavu mjini Asmara. Upande wa pili Eritrea inawaunga mkono ama kundi linaloipinga serikali ya Ethiopaia la Ogaden-National Liberation Front-ONLF, au lile la Oromo, Oromo Liberation Front –OLF.
Annette Werber ,mtaalamu wa masuala ya pembe ya Afrika kutoka taasisi ya sayansi na siyasa mjini Berlin, anaonya juu ya hatari ya kupamba moto kwa hali ya mambo katika mpaka wa nchi hizo mbili jirani akisema ,“Nafikiri tulichokiona mara kwa mara,mwaka jana, daima kumekua na kushutumiana kwamba mmoja anapanga hujuma za kigaidi dhidi ya nchi nyengine. Wameamua kurudi kushutumiana na nafikiri ni ishara kwamba tunapaswa kuwa na tahadhari.”
Tangu majuma kadhaa, kumekuwepo na ripoti za kuimarishwa nyendo za kijeshi katika eneo la mpaka wa kilomita 1000 na baadhi ya mashahidi mjini Addis ababa wametaja juu ya kutumwa kwa ndege na magari ya kijeshi katika eneo la kaskazini. Wengine wanayaangalia matukio ya Ethiopia kuingia Somalia na kuwaangusha viongozi wa mahakama za kiislamu, kuwa ni maandalizi ya vita vipya dhidi ya Eritrea.
Wadadisi wanaashirai kwa upande mwengine kwamba, hali hiyo inaweza kupukwa kwa msaada wa nchi jirani kama vile Jumuiya ya maendeleo ya mashariki na pembe ya Afrika IGAD, kujaribu kupatanisha. Bibi Werber anasema ,“Sioni nchi za eneo hilo zikikubali kuziona Ethiopia na Eritrea zikipigana. Natumai kuna mbinyo zaidi kwa viongozi wa nchi hizo mbili, kwamba hakuna uwezekano kwao kuingia katika duru mpya ya vita.”
Uhusiano baina ya majirani hao wawili katika pembe ya Afrika, Ethiopia na Eritrea umekua si mzuri tangu muda mfupi tu baada ya Eritrea kujipatia huru wake kutoka Ethiopia 1993, baada ya kumalizika vita vilivyodumu miaka 30.