Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vyasitishwa
21 Mei 2018Haya yanakuja wakati ambapo nchi hizo zinapanga mikakati ya makubaliano mapana ya kibiashara. Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin, na mshauri wa kibiashara wa Rais Donald Trump, Larry Kudlow, wamesema makubaliano hayo yaliyoafikiwa na maafisa wa China na Marekani yameweka mkakati wa kuangazia mapungufu ya kibiashara katika miaka ijayo.
Jumamosi, China na Marekani zilisema zitaendelea kuzungumza kuhusu hatua ambazo zitaifanya China kununua bidhaa zaidi za nishati na kilimo kutoka kwa Marekani ili kupunguza hasara ya bidhaa na huduma ya dola bilioni 335 ya kila mwaka baina ya Mareani na China.
Ila katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox huko Marekani, Waziri Mnuchin alisema "tunavisitisha vita vya kibiashara. Kwa hiyo, sasa, tumekubaliana kusitisha vitisho vya ushuru tulivyowekeana tunapojaribu kuufanyia kazi mkakati," alisema Mnuchin. "Rais amekuwa wazi kabisa tangu mkutano wa kwanza na Rais Xi kule Mar-a-Lago, kwamba tutaipunguza hasara ya biashara," aliongeza Mnuchin.
China imedhamiria kuongeza ununuzi wa bidhaa za Marekani
Mnuchin amesema wanatarajia kuona ongezeko kubwa la kati ya asilimia 35 hadi 45 mwaka huu pekee, la mauzo ya kilimo ya Marekani kwa China. Mnuchin pia ametabiri kuongezeka maradufu kwa bidhaa za nishati za Marekani kwa soko la China, ambapo mauzo ya bidhaa hizo yataongezeka kwa kati ya dola bilioni 50 hadi 60 katika kipindi cha miaka mitatu hadi mitano.
Katika taarifa ya pamoja ya China na Marekani, China imedhamiria kuongeza pakubwa ununuzi wake wa bidhaa na huduma za Marekani kwa kusema, ongezeko hilo litayakidhi mahitaji yanayoongezeka ya watu wa China na mahitaji ya ustawi wa kiuchumi wa hali ya juu.
Gazeti rasmi la China, China Daily, limesema kila mmoja ana afueni sasa na kumnukuu kiongozi mkuu wa majadiliano wa China, Naibu Waziri Mkuu Liu He, akisema majadiliano yalikuwa mazuri na yaliyozaa matunda.
Lakini wataalam na wachambuzi wanaamini kwamba pande hizo mbili zimefikia makubaliano ya sasa katika masuala ya muda mfupi tu na hii haimaanishi kwamba vitishi vya kuongezwa kwa ushuru vitaondolewa kabisa. Shi Yinghong ni Mkurugenzi katika Kituo cha Masomo kuihusu Marekani kwenye Chuo Kikuu cha Renmin.
Mafanikio yoyote lazima yatawahusisha marais wa Marekani na China
"Kitisho kikubwa cha vita vya kibiashara kati ya Marekani na China kimedhibtiwa pakubwa, ambalo ni jambo zuri," alisema Shi. "Lakini kwa upande mwengine, kutokana na tofauti zilizoko baina ya China na Marekani na mikakati ya utawala wa Rais Trump, nina hofu kwamba ni makubaliano ya muda tu na hayatadumu kwa muda mrefu," aliongeza Mkurugenzi huyo.
Wachambuzi wanasema iwapo kutakuwa na mafanikio yoyote ya muda mrefu katika mazungumzo ya China na Marekani, basi yatawahusisha marais wa nchi hizo mbili katika kipindi cha mapukutiko kabla uchaguzi wa Novemba.
Rais Trump alifanya kampeni mwaka 2016 akiahidi kuwa mkali kwa China na washirika wengine wa marekani katika biashara. Anaona hasara ya biashara ya Marekani kwa China kama thibitisho kwamba China inafanya biashara chafu na kwamba iliuzidi ujanja tawala zilizopita za Marekani.
Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/APE
Mhariri: Mohammed Khelef