1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita kati ya Taliban na serikali, nchini Pakistan vyaingia wiki ya pili.

12 Mei 2009

Kundi la wanajeshi maalum wa Pakistan au komandos sasa ndio wanaoendeleza mapambano dhidi ya wapiganaji wa kitaliban katika, mabonde huko jimbo la SWAT.

https://p.dw.com/p/Hoih
Wanajeshi wa Pakistan sasa waingia katika mabonde SWAT kuwasaka WatalibanPicha: AP


Mamia kwa maelfu ya raia wa Pakistan nao wanaendelea kuondoka eneo la vita, kuepuka mashambulizi, huku shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi likisema watu milioni moja na laki tatu ni wakimbizi.


Im Flüchtlingslager Mardan Pakistan Menschen flohen aus dem Swat Tal
Raia milioni 1.3 wametoroka vita SWAT.Picha: AP

Leo ni siku ya 16 na jimbo la SWAT nchini Pakistan limegeuzwa uwanja wa vita. Wakaazi wa jimbo hilo sasa ni wakimbizi, kwani wamekuwa wakiondoka eneo la vita- majeshi ya serikali na wapiganaji wa Kitaliban hawajapumzisha vita hivy vya wiki mbili sasa.


Taarifa za kijeshi kutoka Pakistan zinasema jinsi hali ilivyo, wanajeshi maalum au komandos ndio sasa wapo katika safu ya mbele kuingia katika mabonde na ngome za wapiganaji wa Kitaliban huko SWAT.


Meja -Jenerali Athar Abbas, katika mkutano na waandishi wa habari, alisema wanajeshi sasa wameingia katika mabonde katika mji mkuu wa SWAT, Mingora, kuwasaka Wataliban na kuvuruga mitandao yao ya vita.


Huku wanajeshi hao maalum wakiendeleza mashambulizi ya chini kwa chini- ndege za kivita zilikuwa na kazi ya kurushia mabomu maficho ya Wataliban huko Malam na Jabaa.


Kwa wiki mbili sasa Pakistan imeyaripua maeneo ya mafunzo ya Wataliban, nyumba zao na maskani yao- Vita Pakistan inasema ni vya kufa na kupona kuondoa kile Marekani inadai ni mizizi ya ugaidi nchini humo. Taarifa za kijeshi zinasema hadi sasa wapiganaji 751 wa kitaliban wameua katika vita hivi- katika maeneo ya Buner, Dir na katika jimbo la SWAT. Idadi ya wanajeshi waliouawa inasemekana ni 29.


Pakistan Flüchtlinge aus dem Swat Tal
UNHCR inawasiwasi swala la kuwakimu wakimbizi Pakistan litakuwa gumu.Picha: AP

Lakini si vifo tu ndio sasa jumuiya ya kimataifa ina wasiwasi navyo. Swala la kibinadamu linaikodolea macho Pakistan. Watu milioni moja na laki tatu wanasemekana sasa ni wakimbizi baada ya kulikimbia eneo la vita. Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi, UNHCR, limesema hadi sasa watu laki tano ndio waliojiandikisha rasmi kuwa ni wakimbizi tangu mwishoni mwa wiki.


Mashirika ya kutetea haki za raia yameiisihi Pakistan izue kushambulia maeneo yanayokaliwa na raia- ambao bado hawajafanikiwa kuondoka.


Pakistan imekuwa ikikabiliana na wapiganaji wa Kitaliban kaskazini mwa nchi hiyo kwa mwaka wa pili sasa-Serikali ya Asif Zardari ilitia saini makubaliano ya amani na wapiganaji wa kitaliban kumiliki jimbo la SWAT mapema mwaka huu. Lakini wiki mbili zilizopita, kutokana na msukumo wa Marekani kuwa Taliban ni tishio kwa Pakistan, taifa lenye silaha za kinuklia, Pakistan ikauvunjilia mbali mkataba huo na sasa imeapa kuwaangamiza Wataliban nchini Pakistan.


Mwandishi: Munira Muhammad/ afp

Mhariri: Othman Miraji