Virusi vya corona Ukanda wa Gaza: Juhudi za kuepusha janga
Kilichohofiwa muda merefu kimewadia — Ugonjwa wa COVID-19 umeingia katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa. Kila juhudi inafanyika kujaribu kuzuia mripuko na kusimamisha janga.
Vita dhidi ya virusi vya corona
Maambukizi ya virusi vya corona yamefika katika Ukanda wa Gaza, mojawapo ya sehemu zenye msongamano mkubwa sana wa watu duniani. Tayari dazeni ya visa vya COVID-19 imekwishathibitishwa. Kwenye ukanda huo wenye ukubwa wa KM 365 za mraba wanaishi watu wapatao milioni 2, sawa na watu 6,000 kwa kila KM mraba. Kama tahadhari, wafanyakazi wameanza kupulizia dawa ya kuuwa vimelea katika baadhi ya maeneo.
Vituo vya Karantini Gaza
Watu zaidi ya 1,860 waliorejea kutoka ng'ambo wamewekwa karantini katika vituo 26 vya muda. Kituo kimoja kipo karibu na kivuko cha mpakani cha Rafah, na wengine wamewekwa mashuleni ambako watu hukaa kwa siku 21. Kivuko kwenye mpaka wa Misri na Israel kimefungwa kuanzia katikati mwa Machi, na wanaoruhusiwa kupita ni wale tu wanaoingia katika Ukanda wa Gaza
Huduma duni za afya
Ingawa baadhi ya vituo vinavyo vifaa vya kitabibu, huduma za afya katika Ukanda wa Gaza zimekwama. Kuna machine 68 tu za kusaidia watu kupumua, na vitanda 68 katika wodi ya wagonjwa mahatuti. COGAT, mamlaka ya kijeshi ya Israel inayohusika na masuala ya kiraia ya Wapalestina, imesema imepeleka huko vifaa 1,500 vya kupima COVID-19 vilivyotolewa na WHO.
Barakoa zenye michoro ya kuvutia
Wizara ya afya imetangaza hali ya dharura. Wasanii wa Kipalestina Samah Saed (pichani) na Dorgham Krakeh huweka michoro ya rangi za kuvutia kwenye barakoa za kufunika midomo na pua, ili kuwashawishi wenyeji kuzivaa. Ikiwa kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza litashindwa kudhibidi maambukizi ya virusi vya corona, yumkini athari zitakuwa mbaya sana.
Lazima kuhakikisha njia za upatikanaji wa bidhaa muhimu
Matokeo ya kufungwa shughuli zote yatakuwa kama hukumu ya kifo kwa watu wa Ukanda wa Gaza. Asilimia 75 ya wakaazi ni wakimbizi, ambao hutegemea msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Wakimbizi Wapalestina, UNRWA, ambalo bado linagawa chakula nyakati za mchana. Lakini kuanzia saa 11 jioni hadi mapambazuko, watu wanalazimika kubaki nyumbani.
Elimu kwa watoto
Kwa sehemu kubwa, shughuli za kijamii zimesimamishwa. Hata hivyo, wito wa watu kutosogeleana na kuheshimu kanuni za usafi hauitikiwi ipasavyo, hususan katika mitaa miembamba na katika kambi za wakimbizi. Wanaharakati huvaa nguo zinazoonekana kama kirusi ili kuweza kuuelimisha umma wa Palestina ambao wengi wao ni vijana.
Msaada kutoka Qatar
Kundi la Hamas linaendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Qatar, na nchi hiyo ndogo ya ghuba imeahidi kuendelea kuwasaidia kifedha watu wa Gaza. Wiki iliyopita, Qatar ilipeleka dola milioni 10 katika Ukanda wa Gaza. Inaelezwa kuwa kila familia maskini itapokea dola 100.
Baki nyumbani
Kulingana na makadirio ya WHO, vituo vya afya kwenye Ukanda wa Gaza vinao uwezo wa kuwatibu wagonjwa 100 wa kwanza wa COVID-19. Baada ya hapo eneo hilo litalazimika kutegemea msaada kutoka nje. Hiyo ndio sababu wanaharakati na wasanii wanawahamasisha watu kubakia nyumbani kwao.
Keki, kampeni na virusi vya corona
Duka moja la keki katika kitongoji cha Khan Younis kinatoa mchango wake wa kuuelimisha umma, kwa kutengeneza keki zilizovaa barakoa, ili kuwasaidia watu kuulewa mripuko huu.