1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Virusi vipya vya corona vyatishia kufungwa mipaka Ulaya

21 Januari 2021

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watajadili changamoto zinazozidi kuongezeka zinazosababishwa na virusi vipya vya corona, wakati Ujerumani ikitishia kufunga mipaka iwapo mataifa jirani hayatadhibiti maambukizi.

https://p.dw.com/p/3oE0G
Symbolbild EU - China
Picha: Yves Hermann/AFP

Viongozi wa Umoja wa Ulaya hii leo wataangazia namna ya kushughulikia changamoto zinazozidi kuongezeka zinazosababishwa na janga la virusi vya corona kuanzia kudhibiti kusambaa zaidi kwa maambukizi ya virusi vinavyobadilika hadi kitisho kwa kufunga mipaka lakini pia kasi ndogo ya utoaji wa chanjo kote barani Ulaya.

Wakuu wa taasisi za Umoja wa Ulaya wamewaomba viongozi wa mataifa wanachama kuhakikisha wanaimarisha mshikamano na hatua za upimaji pamoja na utoaji wa chanjo ingawa bado hakuna matarajio ya hitimisho rasmi kupitia mkutano wa wakuu hao unaofanyika kwa njia ya video ambao ni wa tisa tangu kuanza kwa janga hilo.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imesema Jumanne hii kwamba mataifa 27 ya umoja huo yatatakiwa kuwa yametoa chanjo kwa angalau asilimia 70 ya watu wazima hadi ifikapo majira ya joto.

Mataifa ya Ulaya yameelezea wasiwasi, baada ya wiki iliyopita kugundua kwamba chanjo ya Pfizer inayozalishwa na mmoja kati ya wazalishaji wawili waliothibitishwa na Umoja wa Ulaya huenda ikapunguza kiwango cha usambazaji. Italia inaangazia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya hatua hiyo ya Pfizer.

Deutschland Coronapandemie Pressekonferenz Bundeskanzlerin Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atishia kufunga mipaka iwapo majirani zake hawatadhibiti kikamilifu kusambaa kwa virusi vipya vya corona.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture-alliance

Huku hayo yakiendelea, kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ameonya Jumanne kwamba nchi yake ambayo iko chini ya vizuizi vya kufunga shughuli itahitaji kuliangazia suala la kufunga mipaka iwapo mataifa mengine hayakuchukua hatua za kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi vipya vya corona.  

Tukiacha na yanayoendelea Ulaya, nchini Marekani, rais Joe Biden. Biden amesaini amri 17 za rais katika siku yake ya kwanza madarakani, na miongoni mwa amri hizo alizozipatia kipaumbele cha kwanza lilikuwa ni ya kupambana na janga hilo nchini mwake, ambalo hadi sasa limewaua watu 405,000 na zaidi ya watu milioni 24 wakiwa wameambukizwa. Kwenye amri hiyo amewataka watu kuvaa kwa lazima barakoa.

"Na amri ya kwanza nitakayosaini hapa inahusiana na COVID-19 na kama nilivyosema wakati wote tutawataka watu wavae barakoa kwenye majengo ya serikali na kuzingatia umbali. Na ya pili ninayosaini hapa ni msaada kwa jamii ambazo hazipati huduma nzuri na tunapaswa kuhakikisha kuwa tunakuwa na usawa wa msingi kuhusu jinsi tunavyowahudumia watu katika huduma za afya na mambo mengine. Alisema Biden.

Nchini China, katika jiji la Shanghai mamlaka zimeanza kuwahamisha wakaazi wa maeneo jirani baada ya maafisa nchini humo kugundua angalau visa vitatu vya virus vipya vya corona hii leo. Maafisa hao hata hivyo hawakusema ni watu wangapi hasa wameondolewa kwenye maeneo hayo, katikati ya jiji la Shanghai wakati wakiimarisha zaidi upimaji kufuatia mripuko huo.

Na huko Geneva, Uswisi, shirika la Afya ulimwenguni WHO limeishukuru serikali mpya ya rais Joe Biden kwa hatua yake ya haraka ya kuirejesha Marekani kwenye shirika hilo, baada ya rais aliyeondoka Donald Trump wa kuiondoa.

Mwanasayansi mwandamizi wa Marekani Anthony Fauci amesema pia kwamba Marekani inataka kurejea tena kwenye majukumu yake ya kuwa mfadhili mkubwa zaidi kwenye shirika hilo. Fauci ambaye ameteuliwa na Biden kama mshauri mkuu wa masuala ya afya, ameuambia mkutano wa bodi ya utendaji ya shirika hilo mjini Geneva.

Mashirika: AFPE/APE