Hisia zatolewa kuhusu mkataba wa nyuklia
16 Julai 2015Rais Barack Obama amesifu makubaliano ya kihistoria ya kinyuklia na Iran leo na kusema ni fursa kwa mahasimu hao wa siku nyingi kuelekea katika "mwelekeo mpya", wakati huo huo akilionya baraza la Congress la Marekani kwamba itakuwa halijawajibika iwapo litazuwia makubaliano hayo.
"Kutokupatikana makubaliano ina maana nafasi kubwa kwa vita zaidi katika mashariki ya kati," Obama amesema baada ya kupatikana makubaliano hayo. Obama ameongeza kwamba makubaliano hayo hayakujengeka kwa misingi ya uaminifu, lakini yamejengeka katika uchunguzi.
"Tofauti zetu ni za kweli. Historia ngumu baina ya mataifa haiwezi kupuuzwa. Inawezekana kubadilishwa, " amesema Obama. "Makubaliano haya yanatoa fursa kusonga mbele katika mwelekeo mpya . Tunapaswa kuikumbatia. Rais wa Marekani hata hivyo ameahidi kuendelea na juhudi zote kuimarisha usalama wa Israel, juhudi ambazo zinapindukia kile ambacho utawala wowote wa Marekani umeweza kufanya hapo kabla.
Viongozi wengi wayaunga mkono makubaliano
Mgombea urais wa chama cha Republican Marco Rubio amesema anatarajia baraza la Congress kupiga kura dhidi ya makubaliano hayo na Iran, akisema makubaliano hayo yanadhoofisha usalama wa Marekani.
Rais wa Iran Hassan Rouhani amewaambia Wairan katika hotuba kwamba "malengo yetu yote" yamefikiwa katika makubaliano haya.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema kwamba makubaliano ya kinyuklia ni hatua kuelekea kujitoa katika mzozo na pia kuenea kwa silaha za kinyuklia.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza Philip Hammond amesema kwamba kazi ya urutubishaji wa madini ya urani kwa kiasi fulani pamoja na shughuli za maendeleo katika mradi huo unairuhusu Iran kuwajibika katika makubaliano haya na haitaleta kitisho cha Iran kuweza kutengeneza silaha za atomic.
"Tunaimani kwamba fursa chache ambacho zinapatikana kwa Iran chini ya makubaliano haya zitaweka kurefusha muda wa kuweza kutayarisha mafuta ya kinyuklia kuweza kutengeneza silaha za atomic , kitu ambacho kilikuwa muhimu katika matarajio yetu" amesema waziri wa Hammond.
Kwa wakosoaji , kuondoa vikwazo dhidi ya Iran chini ya makubaliano haya ya kihistoria kutasaidia kuipa uwezo Iran kuchochea hali ya machafuko katika mashariki ya kati , lakini baadhi ya wataalamu wanasema suala la nyuklia limekuzwa mno badala ya kuangalia mizozo ya hivi sasa katika eneo hilo.
Makubaliano haya yamekuja baada ya karibu muongo mmoja wa diplomasia kimataifa na kati ya mabara ambayo hadi hivi karibuni ilikuwa ikikabiliwa na kushindwa tu.
Marekani imejiunga na majadiliano mwaka 2008, na maafisa wa Marekani na Iran walikutana kwa siri miaka minne baadaye nchini Oman kuona iwapo hatua za kidplomasia zinawezekana.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman