Viongozi wataka kuwe na utaratibu mkali kuyalinda mazingira
28 Aprili 2020Kinachopendekezwa na waziri huyo wa mazingira wa Ujerumani ambaye ni mwanasiasa kutoka chama cha SPD pamoja na wengine kwenye mkutano huo, ni kuwepo mwanzo mpya wa kulinda mazingira baina ya jamii na taasisi baada ya janga la virusi vya Corona duniani.
Mazungumzo hayo kwa njia ya video yaliyoanza jana Jumatatu yanaunga mkono mpango wa kiuchumi wa kuimarisha mazingira na ambao utatoa fursa ya kuwepo mwanzo mpya katika utunzaji wa mazingira duniani ambapo suala la kupunguzwa kwa uzalishaji wa gesi inayochafua mazingira litabidi kuchukua dira ya kushughulikiwa kwa kiwango sawa.
Mtazamo huo uliosisitizwa na Waziri wa Mazingira Schulze umeungwa mkono pia na kiongozi wa Chama cha Watetezi wa Mazingira cha Kijani, Annalena Baerbock, ambaye amezungumzia juu ya kuwepo mpango wa kiuchumi utakaovibana viwanda kuwekeza katika ulinzi wa mazingira.
Waziri Schulze, kwa upande mwingine, amesisitiza kwamba tafauti na mapambano dhidi ya virusi vya Corona, chanjo ya kuutatua mgogoro wa kimazingira inajulikana, inapatikana na gharama zake inawezekana kuzimudu.
Mfano aliozungumzia waziri huyo ni pamoja na kutumiwa nishati ya upepo, na jua pamoja na magari au usafiri wa kutumia umeme na kutilia mkazo ujenzi wa majengo unaozingatia kwa kiasi kikubwa mazingira.
Kwa mtazamo waziri huyo, itakuwa rahisi kuuzuia mgogoro wa kimazingira huku akisisitiza pia kwamba suala la ulinzi wa mazingira sio suala linalohusu ufahari.
Ikumbukwe kwamba mkutano huu wa kimataifa wa kuhusu mazingira kwa mara ya kwanza umefanyika kwa njia ya video kutokana na janga la Corona ukiwaunganisha mawaziri na wanasayansi pamoja na mashirika kutoka takriban nchi 30, zikiwemo China, India, Japan na nchi za Umoja wa Ulaya na nchi za visiwa zilizo kwenye hatari ya kuathirika pamoja na Ethiopia.
Mkutano huo utafungwa kwa matamko kutoka kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Mkutano huo wa mwaka huu umeandaliwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Ujerumani na Uingereza.