Viongozi wahutubia mkutano wa usalama wa Munich
20 Februari 2017Kansela Angela Merkel amesema kwamba hatari kama ile inayotokana na magaidi wanaojiita Dola la Kiislamu IS haiwezi kuzuiwa na nchi moja peke yake, na kwa hivyo ametoa mwito wa kujengwa mfumo wa pamoja duniani ili kuikabili hatari hiyo. Kiongozi wa Ujerumani pia aliwaambia wajumbe kwenye mkutano wa mjini Munich kwamba pana ulazima wa kuboresha na kuoanisha mashirika ya kimataifa kama vile Umoja wa Ulaya. Bibi Merkel amesema kuwa taasisi hizo ni muhimu sana na ndio sababu pamoja na mambo mengine ameusisitiza msimamo thabiti wa Umoja wa Ulaya katika jumuiya ya ulinzi ya NATO. Merkel ameahidi kwamba Ujerumani itajitahidi ili kulifikia lengo lililowekwa la kuchangia asilimia mbili ya pato jumla la nchi yake kwa ajili ya bajeti ya ulinzi ya jumuiya ya NATO. Hata hivyo kansela Merkel amekumbusha kwamba jumuiya hiyo ni muhimu sio tu kwa Ulaya bali pia kwa Marekani vilevile.
Hotuba ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel ilifuatiwa na ile ya makamu wa rais wa Marekani Mike Pence aliyewahakikishia washirika wa barani Ulaya kwamba Marekani itaendelea kusimama nao kwa uthabiti katika jumuiya ya NATO. Hata hivyo makamu wa rais wa Marekani Mike Pence amezitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo pia zitoe mchango wao kwa haki. Bwana Pence amesema wakati sasa umefika wa kuchukua hatua zaidi ili kupambana na changamoto za kijeshi mbalimbali zilizopo sasa duniani.
Makamu wa rais wa Marekani ameeleza kwamba ukiiondoa Marekani na nchi nyingine nne tu wanachama wa NATO hakuna nchi nyingine iliyolifikia lengo la kuchangia asilimia mbili ya pato jumla la taifa kwa ajili ya bajeti ya NATO. Bwana Pence amesema kwamba nchi yake sasa inapanga kuwa na nguvu kubwa zaidi za kijeshi kuliko hapo awali.
Changamoto zinazoikabili NATO
Pamoja na changamoto zinazoikabili NATO makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ameitaja hali ya mashariki mwa Ulaya ambapo amesema Urusi inajaribu kuibadilisha mipaka ya kimataifa. Bwana Pence ameeleza kwamba nchi yake itaendelea kuilaumu Urusi lakini wakati huo huo itajaribu kutafuta maslahi ya pamoja.
Msimamo wa Marekani juu ya NATO ulitiliwa mashaka na rais Donald Trump aliyesema kwamba jumuiya hiyo imeshapitwa na wakati ingawa katika siku za hivi karibuni zimetolewa kauli za kuwapa uhakika washirika wa barani Ulaya. Baada ya hotuba yake makamu wa rais wa Marekani Mike Pence alikutana kwa faragha na kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Wakati huo huo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katibu mkuu wa NATO Jen Stoltenberg na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov wanatarajiwa kutoa hotuba kwenye mkutano huo wa mjini Munich.
Kwa mujibu wa habari leo alasiri wapinzani wa mkutano huo wa mjini Munich wanatarajia kufanya maandamano ambapo watu hadi 4000 wanatazamiwa kushiriki. Mkutano huo wa mjini Munich unahudhuriwa na wanadiplomasia pamoja na wadau wa maswala ya usalama kutoka nchi mbalimbali.
Mwandishi: Zaainab Aziz/APE/RTRE/AFPE
Mhariri: Buwayhid Yusra