Viongozi wa Umoja wa Ulaya wagawika kuhusu bajeti
24 Februari 2018Rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema viongozi ho wa mataifa 27, wanaokutana bila ya Uingereza kujadili mipango ya baadaye , wanataka kuchangia zaidi kuhusu ulinzi, uhamiaji na usalama.
Lakini hawakuafikia juu ya iwapo nchi hizo zitalipia katika bajeti ya pamoja kuziba pengo linaloachwa wazi baada ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo yaani Brexit la euro bilioni 15 kwa mwaka.
"Nchi nyingi ziko tayari kuchangia zaidi katika bajeti hiyo ya kabla ya mwaka 2020," Tusk aliwaambia waandishi habari, na kuongeza kwamba "wanahitaji kutatua suala hilo la pengo la bajeti linalosababishwa na Brexit".
Mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker amesema mataifa 14 ama 15 yamekubali kuongeza mchango wao wa taifa, hali ambayo bado inaacha karibu nusu ya mataifa ya kundi hilo bado hayajaamua ama kupinga.
"Mjadala haukuwa wa malumbano zaidi kama nilivyotarajia," amesema Juncker , akionya hata hivyo kuwa :"Iwapo hakuna fedha nyumbani mapenzi yanapeperuka nje ya mlango." Nchi muhimu kiuchumi kama Ujerumani, Uhispania na Ufaransa ziko tayari kulipa zaidi.
Upanuzi wa bajeti
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwaambia waandishi habari kuwa Ufaransa iko tayari kupanua bajeti yake. Waziri mkuu wa uhispania Mariano Rajoy aliongeza: "nafikiri Uhispania inapaswa kuwa wazi na kutumbukiza rasilmali nyingi zaidi." Lakini upinzani unaongozwa na Uholanzi, Denmark, Sweden na Austria, nchi ambazo ni "wachangia wakubwa" ambao wanalipa zaidi katika bajeti ya Umoja wa Ulaya kuliko zinavyopata.
"Kile tusichokitaka ni mzigo wa ongezeko la kila mara katika matumizi," Kansela wa Austria Sebastian Kurz alisema.
Wakati huo huo, Umoja huo umetoa kwa baadhi ya mataifa sita ya eneo la Balkan ambayo yana matumaini ya kujiunga na kundi hilo la mataifa uwezekano wa kuwa wanachama ifikapo mwaka 2025, lakini umezionya nchi hizo kwamba bado zina vikwazo vya kuvuka.
Mwongozo wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya eneo hilo uliowasilishwa mapema mwezi huu unasena nchi hizo ni lazima ziondoe matatizo yanayohusiana na rushwa na utawala wa sheria na hususan kutatua mizozo kadhaa inayotokota ya mipaka.
Mlango uko wazi
Mlango wa Umoja wa Ulaya uko wazi kwa kuwaingiza pale tu , nchi moja moja zitakapotimiza masharti ," mpango huo umesema.
Mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker ataanza zira ya eneo hilo kesho Jumapili kujadili mkakati mpya, ambao unasisitiza "utekelezaji wa mageuzi ya msingi pamoja na mahusiano mazuri ya ujirani".
Montenegro na Serbia ni nchi zilizoko mbele kujiunga pamoja na Albania, Bosnia , Kosovo na Macedonia zikiwa nyuma, lakini zote zinaingiwa na wasiwasi baada ya Umoja wa Ulaya kuzuwia upanuzi miaka minne iliyopita.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Caro Robi