Umoja wa Ulaya wafikia makubaliano kuhusu uhamiaji
29 Juni 2018Mpango huo wa maelewano uliofikiwa mapema asubuhi ya leo unakuja baada ya majadiliano yaliyodumu kwa muda wa masaa zaidi ya 12, wakati viongozi hao walipokutana katikati mwa ongezeko la shinikizo la kutafuta ufumbuzi wa tatizo la uhamiaji, unaonekana kuhatarisha mustakabali wa umoja huo.
Mpango huo ni ushindi kwa Italia, inayoongozwa na waziri mkuu Giuseppe Conte, ambaye amekuwa akisukuma ajenda ya kugawana mzigo wa wahamiaji miongoni mwa nchi wanachama na hata kutishia kutumia kura yake ya turufu katika maamuzi ya mkutano huo wa kilele hadi pale viongozi wake wangefikia makubaliano ya pamoja juu ya uhamiaji. "Kwa hiyo naweza kusema kwa ujumla tunaweza kuridhika. Yalikuwa majadiliano ya muda mrefu lakini kuanzia leo Italia haiko peke yake," alisema Conte.
Serikali ya Conte ya mrengo mkali wa kulia imekuwa ikichochea mjadala wa uhamiaji Ulaya kwa kufunga bandari zake dhidi ya meli mbili zilizowaokoa wahamiaji katika wiki zilizopita, na kutaka mabadiliko makali katika sera ya Uhamiaji ya Ulaya.
Chini ya makubaliano haya mapya, nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zitaanzisha kwa hiari yake vituo vya udhibiti katika ardhi yake kushughulikia wahamiaji waliookolewa baharini.
Wale wanaostahili ulinzi wa kimataifa watagawanywa miongoni mwa nchi wanachama ambao watawachukua wahamiaji kwa hiari. Hii itaiondolea mzigo Italia, ambayo kwa sasa inashughilikia wahamiaji wengi waliokolewa kwenye bahari ya Mediterenia.
Muungano huo pia utafanyia kazi kwa haraka dhana ya majukwaa ya utengano wa kikanda yatakayokuwa ni vituo vya kushughulikia wahamiaji nje ya Ulaya, uwezekano mkubwa ikiwa ni Afrika ya kaskazini. Kwa hili Umoja wa Ulaya utahitaji idhini kutoka nchi nyingine zinazohusika.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameyasifu makubaliano hayo akisema licha ya kazi kubwa inayotakiwa kufanywa kabla ya ukanda huo haujafikia msimamo wa pamoja wa waomba hifadhi, lakini ana matumani kwamba kuanzia leo wataendelea na kazi.
"Tumekubaliana juu ya miongozo mitano lakini miwili bado inakosa mfumo wa pamoja wa Ulaya wa waomba hifadhi lakini nina matumaini baada ya leo tunaweza kuendelea kufanya kazi ingawa kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuunganisha mitazamo tofauti, alisema Merkel.
Merkel amekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer ambaye amempatia muda wa mwisho wa hadi mwishoni mwa Juni ili apunguze idadi ya waomba hifadhi wanaiongia Ujerumani au ahatarishe serikali yake ivunjike.
Kansela wa Austria Sebastian Kurz amesema mpango huo utaiwezesha Umoja wa Ulaya kulinda mipaka yake kwasababu kwa mara ya kwanza kuna uwezekano wa kufunguliwa vituo nje ya Ulaya. Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesifu mpango huo akiuita ufumbuzi wa Ulaya na matunda ya kazi ya pamoja. Amesema hii ni bora zaidi ya suluhisho la nchi moja moja, ambalo lisingefikiwa hata hivyo. Nchi hizo zimekubaliana kuongeza nyongeza ya yuro milioni 500 kuzisaidia nchi za afrika.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa
Mhariri: Josephat Charo