Viongozi wa ulimwengu wakipata chanjo ya COVID - katika picha
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amejiunga na orodha inayoongezeka ya viongozi wa ulimwengu ambao wamepewa chanjo dhidi ya COVID-19. Huu hapa muhtasari wa wale ambao wamepata chanjo hadi sasa.
Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden alipatiwa chanjo yake ya pili ya BioNTech-Pfizer mnamo Januari. Kulingana na takwimu kutoka Vituo vya Udhibiti na Kuzuia Magonjwa vya Marekani hadi katikati mwa Aprili, karibu watu milioni 120 nchini Marekani wamepatiwa angalau dozi moja ya chanjo. Zaidi ya watu milioni 70 wamepewa chanjo kamili.
Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanjahu pia alipewa chanjo ya BioNTech-Pfizer. Israeli ilipata mamilioni ya chanjo baada ya kuridhia kutoa data za kitabibu kuhusu uwezo wa chanjo ya Pfizer. Kufikia katikati mwa Aprili, karibu 53% ya idadi ya watu milioni 9.3 wa Israeli walikuwa wamepatiwa dozi zote. Israeli kwa kiasi kikubwa imefungua uchumi wake wakati janga hilo linaonekana kupungua.
Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi akidungwa chanjo ya Covaxin COVID-19 iliyotengenezwa na India mnamo Machi 1. India imepanua zaidi utoaji chanjo kutoka kwa wafanyakazi wa huduma ya afya na wafanyikazi wa mstari wa mbele, na kuwachanja wazee na wale walio na matatizo hatari ya kiafya. India sasa ina idadi ya pili ya juu zaidi ya visa ulimwenguni kufuatia kuongezeka kwa maambukizo hivi karibuni.
Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alipatiwa chanjo ya AstraZeneca mnamo Machi. Chanjo iliyotengenezwa na Uingereza imekuwa na utata. Nchi kadhaa zilisitisha matumizi yake kwa hofu kwamba inasababisha kuganda kwa damu.
Jean Castex
Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean Castex alipodungwa chanjo ya AstraZeneca siku moja na Johnson. Alipatiwa chanjo katika tukio lililopeperushwa moja kwa moja kupitia televisheni ili kukuza imani ya umma juu ya chanjo.
Scott Morrison
Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison alipatiwa chanjo ya BioNTech-Pfizer. Morrison mwezi huu alidai kwamba Australia imeizidi Ujerumani, New Zealand na Korea Kusini na ipo katika hatua sawa na Japan katika utoaji chanjo. Lakini ameachana na lengo lake la kuwachanja dozi kamili Waaustralia wote kufikia mwishoni mwa mwaka.
Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan alipatiwa dozi ya chanjo ya Sinovac iliyotengenezwa na China mbele ya kamera za Runinga mnamo Januari. Lengo lilikuwa kupunguza mashaka yoyote ya umma juu ya ufanisi wa chanjo. Uturuki imetoa karibu dozi milioni 19 kufikia sasa, na ilitegemea zaidi chanjo ya Sinovac hadi chanjo ya BioNTech-Pfizer ilipoanza kutolewa Aprili 2.
Joko Widodo
Rais wa Indonesia Joko Widodo ni miongoni mwa waliodungwa chanjo ya Sinovac. Alipata dozi yake ya pili mnamo Januari 27 katika tukio lililorushwa moja kwa moja kupitia runinga. Serikali inakusudia kuwapatia chanjo watu milioni 181.5 ifikapo mwaka ujao.
Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipewa chanjo ya AstraZeneca ya COVID-19 mnamo Aprili, lakini ofisi yake haikutoa picha zozote wakati akidungwa chanj hiyo tofauti na viongozi wengine wa ulimwengu. Ofisi yake badala yake ilitoa picha za hati zinazothibitisha chanjo yake.