Viongozi wa Ulaya wakubaliana mpango wa madeni
29 Juni 2012Hatimaye, baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika hali tete sana na kuendelea hadi alfajiri ya leo, Rais wa Umoja wa Ulaya, Herman Van Rompuy, ameyasifu matokeo ya mazungumzo hayo kama "njia ya uhakika" kuyatulizanisha masoko ya kifedha na kulijenga upya eneo la sarafu ya euro ili kuliepusha na mgogoro mwengine wa kifedha hapo baadaye.
"Tunataka kukamilishwa kwa haraka kwa makubaliano yaliyoambatanishwa kwa msaada wa kifedha kwa Uhispania kuipa fedha sekta yake ya benki na tunathibitisha kuwa msaada wa kifedha utatolewa na Mfuko wa Kuwezesha Utulivu wa Kifedha wa Ulaya hadi pale Mpango wa Utulivu wa Ulaya utakapokuwa tayari." Amesema Van Rompuy.
Makubaliano hayo yanafungua njia kwa mabenki yanayozorota kwenye kanda ya euro kupokea euro bilioni 500 moja kwa moja, bila ya kupitia kwenye bajeti za mataifa hayo. Euro nyengine bilioni 55 zitatolewa kutoka kasma ya fedha za Umoja wa Ulaya ambazo hazijatumika na kuingizwa kwenye biashara za kiwango cha kati na cha chini na miradi ya ajira kwa vijana wa Ulaya.
Fedha za kununua dhamana za madeni
Hatua nyengine muhimu kwenye makubaliano hayo ni kwamba fedha za uokozi zitatumika kwa njia yenye unyumbufu na ufanisi zaidi kwa lengo la kuyatuliza masoko, inayomaanisha kwamba dhamana za nchi zinaweza kununuliwa ili kupunguza gharama za ukopaji, ambazo kwa wiki za hivi karibuni zimezinamia Uhispania na Italia.
Akizungumzia hatua hiyo, waziri wa fedha wa Uhispania, Cristobal Montoro, amesema kwamba nchi yake imejitolea kuufanyia kazi ipasavyo mpango wa uokozi wa Umoja wa Ulaya.
"Utekelezaji wa bajeti inayosawazisha nakisi kwenye matumizi ya sekta ya umma ndio njia moja ya kuonesha kuwa Uhispania na serikali yake imejitolea kuwa na bajeti tulivu. Huu ndio ufunguo wa kujifufua kwa sarafu ya euro. Tunataka tuaminiwe tena." Amesema Montoro.
Merkel asema Ujerumani hakubadilisha msimamo
Akiondoka kwenye mkutano huo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, amesema kwamba wamechukuwa uamuzi mzuri kwa ajili ya ukuwaji wa uchumi.
Licha ya baadhi ya ripoti kuonesha kuwa Merkel aliondosha msisitizo wake kwamba fedha zinazotolewa na mfuko wa uokozi lazima zipitishwe kwenye bajeti za serikali, mwenyewe amewaambia waandishi wa habari kwamba Ujerumani imeendelea kubakia na msimamo wake ule ule wa nipa-nikupe na kutaka lazima pawepo na udhibiti na masharti.
Rais Francois Hollande amesema kwamba kilichopatikana kwenye mkutano huu, ni hatua za pamoja za Umoja wa Ulaya kuelekea kutatua mgogoro wa kifedha.
Viongozi wa Ulaya wamekubaliana pia juu ya hatua kadhaa zenye thamani ya euro bilioni 120 wanazotarajia kusaidia kuinua ukuwaji wa uchumi kwenye eneo la sarafu ya euro. Wameahidi kuongeza mtaji wa benki ya uwekezaji ya Ulaya hadi euro bilioni 10 kwa ajili ya kuongeza uwezo wake wa kukopa hadi euro bilioni 60, na kuzisaidia nchi zilizo kwenye mazingira magumu kujitoa zenyewe kwenye mgogoro wa kifedha.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman