1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ufaransa na Australia wazuru Afghanistan.

23 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CfKV

Kabul. Viongozi wa Ufaransa na Australia wamefanya ziara ambazo hazikutangazwa hapo kabla nchini Afghanistan jana Jumamosi , wakisisitiza kuunga kwao mkono juhudi za serikali ya nchi hiyo dhidi ya magaidi.

Akizungumza mjini Kabul , rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesema kuwa , nchi yake itachukua uamuzi katika wiki chache zijazo iwapo iongeze wanajeshi wake na kuimarisha idadi ya hivi sasa ya wanajeshi 1,600 katika jeshi la kimataifa linalosaidia kuweka usalama , linaloongozwa na NATO.

Waziri mkuu mpya wa Australia Kevin Rudd naye pia alikuwa mjini Kabul. Amewaambia waandishi wa habari baada ya mazungumzo na rais wa Afghanistan Hamid Karzai kuwa nchi yake inataka kujikita nchini Afghanistan kwa muda mrefu zaidi.

Australia ina wanajeshi 900 , wengi wao wakiwa katika eneo lenye machafuko katika jimbo la kusini kati la Uruzgan.