1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Taliban ya Afghanistan wako Pakistan

Iddi3 Machi 2016

Afisa wa ngazi ya juu nchini Pakistan amekiri kuwa viongozi wa kundi la Taliban la Afghanistan wanaishi kwa salama ndani ya Pakistan - karata inayotumiwa kuwashinikiza kuzungumza na serikali ya Kabul.

https://p.dw.com/p/1I6Tl
Wapiganaji wa Taliban wakimsikiliza kiongozi wao Mullah Muhammad Akhtar.
Wapiganaji wa Taliban wakimsikiliza kiongozi wao Mullah Muhammad Akhtar.Picha: Getty Images/AFP/J. Tanveer

Kukiri kwa afisa huyo Sartaj Aziz - mshauri wa mambo ya kigeni wa Pakistan kumekuja baada ya miaka kadhaa ya kukusha kwa serikali ya Pakistan kwamba inatoa hifadhi au ina ushawishi wowote juu ya kundi la Taliban, na wakati ambapo kuna msukumo mpya wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja.

Uasi wa miaka 14 wa kundi la Taliban dhidi ya vikosi vya Afghanistan na jumuiya ya kujihami NATO, umegahrimu maisha ya maelfu ya raia na pia wanajeshi.

Akizungumza katika baraza la mambo ya kigeni mjini Washington siku ya Jumanne, Aziz alisema Pakistan ina ushawishi fulani juu ya kundi hilo kwa sababu viongozi wao wako nchini humo pamoja na familia zao, na wanapatiwa huduma zote za afya, ili waweze kutumia fursa hiyo kuwashinikiza kuja kwenye meza ya mazungumzo.

Kiongozi mkuu wa sasa wa Taliban Mullah Muhammad Akhtar.
Kiongozi mkuu wa sasa wa Taliban Mullah Muhammad Akhtar.Picha: picture-alliance/dpa/Afghan Taliban Militants/Handout

Upatanishi wa Pakistan

Matamshi hayo yanathibitisha kile ambacho kimekuwa siri ya wazi katika nyanja za kidiplomasia, hususani tangu Pakistan ilipoanza kuongoza mazungumzo kati ya Kabul na Wataliban majira ya kiangazi mwaka uliyopita. Majadiliano yalivunjika baada ya idara ya ujasusi ya Afghanistan kuvujisha habari kwamba mwasisi wa kundi hilo Mulla Mohamed Omar alifariki dunia mwaka 2013.

Baadae Wataliban walithibitisha kuwa walidanganya kuhusu kifo cha Omar kwa miaka miwili, na kusababisha miongoni mwa wapiganaji na hasira dhidi ya mrithi wake Mullah Akhtar Mansour kwa kuongoza uongo huo. Wengi wa viongozi wa kundi hilo wanaaminika kuishi katika mji wa kusini-magharibi wa Quetta, na wengine wanaishi Peshwar na kusini mwa Karachi.

Pakistan, Afghanistan, Marekani na China, zilifanya duru yao ya nne ya mazungumzo yanayolenga kufufua mazungumzo ya amani ya ana kwa ana kati ya Kabula na Watalibani mwishoni mwa mwezi uliyopita. Kundi hilo la mataifa manne liliwaalika wawakilishi wa Taliban kurudi kwenye mazungumzo kufikia wiki ya kwanza ya mwezi huu wa Machi, inagawa msemaji wa wapiganaji hao alisema baadaye kuwa hawajapokea mwaliko huo.

Wapiganaji wa Taliban wakimsikiliza kiongozi wao Mullah Muhammad Akhtar.
Wapiganaji wa Taliban wakimsikiliza kiongozi wao Mullah Muhammad Akhtar.Picha: Getty Images/AFP/J. Tanveer

Bado hakuna tarehe ya mazungumzo

Aziz alisema Pakistan ilitumia kitisho cha kuwafukuza ili kuwalaazimisha Wataliban kushiriki mazungumzo ya duru ya kwanza, yaliyofanyika Julai 7.

Aliongeza kuwa jukumu la Pakistan ni la muwezeshaji na ni juu ya serikali ya Kabul kuyafanya mazungumzo hayo yazae matunda.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Pakistan, alisema siku ya Alhamisi wakati wa mkutano wa kawaida na waandishi wa habari, kuwa asingeweza kuzungumzia matamshi ya Azizi.

Msemaji huyo Nafees Zakaria, alisema Aziz alisema alichotakiwa kusema na kwamba wao hawaezi kuzungumzia matamshi ya viongozi wao. Zakaria aliongeza hata hivyo kuwa hakuna tarehe iliyothibitishwa kwa ajili ya mazungumzo na Wataliban, na kuongeza kuwa juhudi bado zinaendelea.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhairiri: Mohammed Abdul-Rahman