1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Sudan Kusini washinikizwa kuumaliza mzozo

Admin.WagnerD7 Novemba 2014

Viongozi wa Afrika Mashariki wamewaonya wanasiasa wakuu wa Sudan Kusini wanaozozana kuwa sharti warejeshe akili zao timamu ili kuumaliza mzozo wa miezi kumi na moja uliolikumba taifa hilo changa

https://p.dw.com/p/1Diof
Picha: Ashraf Shalzy/AFP/Getty Images

Waziri mkuu wa Ethiopia Mariam Hailemariam Desalgen amesema katika mkutano wa kilele wa viongozi wa kanda wanaojaribu kutafuta makubaliano ya amani katika mzozo wa Sudan Kusini kuwa inaonekana kuna hamu ndogo ya kufikia amani ilhali watu wa Sudan Kusini wanaendelea kuwa waathiriwa wakubwa wa mzozo huo.

Hailemariam aliwaambia Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar kuwa wote wawili wanafahamu vizuri kuwa subira ya jumuiya ya kimataifa inazidi kupungua.

Vita vimedumu kwa miezi kumi na moja

Mkutano huo uliofanyika jana uliowaleta pamoja viongozi sita wa nchi za kanda ya jumuiya ya ushirikiano ya nchi za Afrika mashariki na pembe ya Afrika IGAD ambao uliwajumuisha Kiir na Machar unafuatia onyo jipya la baraza la usalama la umoja wa Mataifa wiki hii kuwa itaiwekea Sudan Kusini vikwazo ili kukomesha ghasia ambazo zimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha mamilioni wengine bila ya makaazi.

Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya IGAD wakikutana Addis Ababa kuhusu Sudan Kusini
Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya IGAD wakikutana Addis Ababa kuhusu Sudan KusiniPicha: ZACHARIAS ABUBEKER/AFP/Getty Images

Vita vilizuka mwezi Desemba mwaka jana baada ya Rais Kiir kumfuta kazi Machar kama makamu wake kwa madai ya kupanga njama ya kuipindua serikali na baadaye mzozo huo ukageuka kuwa vita vya kikabila kati ya makabila ya Dinka na Nuer ambavyo vimehusisha makundi ishirini tofauti ya wapiganaji.

Juhudi za mara kwa mara za kupatikana amani na kusitisha mapigano zimeshindwa kurejesha hali ya kawaida katika taifa hilo changa.Haile Mariam amesema watatumia ushawishi wao kuhakikisha pande hizo mbili zinazozozana zinakuwa na akili ya kutambua mzozo huo hautakuwa na matokeo ya tija.

AU yasema ni wajibu wake kukomesha vita

Rais wa halmashauri ya umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma ambaye alihudhuria mkutano huo amesema wana wajibu kwa watu wa Sudan Kusini kuzihimiza pande zote mbili kujali maslahi ya raia wake kwa kukomesha umwagikaji damu na kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini humo.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini ZumaPicha: Reuters

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni wa kutoka Djibouti, Kenya, Somalia, Sudan na Uganda ambao wote ni wanachama wa IGAD ambayo inasimamia mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini.

Marekani iliyounga mkono Sudan Kusini kuwa taifa huru miaka mitatu iliyopita imezionya pande zinazozozana kuwa wanahitaji kujitoa muhali kuhakikisha amani inarejea.

Mjumbe wa Marekani kuhusu Sudan Kusini Donald Booth alisema kabla ya kuanza kwa mkutano huo uliokuwa ukifanyika Addis Ababa Ethiopia kuwa amani inahitaji uwajibikaji wa madhila yaliyofanywa ili kiu cha kisasi kiweze kukidhiwa.

Ethiopia, Kenya na Uganda zimelazimika kuwahifadhi zaidi ya wakimbizi 467,000 wa Sudan Kusini waliotoroka vita hivyo na Uganda imeyatuma majeshi yake kulisaidia jeshi la Rais Kiir huku Kenya na Ethiopia zikituma majeshi kuwa sehemu ya kikosi cha umoja wa Mataifa cha kulinda amani.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri: Yusuf Saumu