1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Sudan Kusini kufikia makubaliano kamili leo

17 Agosti 2015

Pande zinazozana nchini Sudan Kusini zinafanya mazungumzo ya kutafuta amani katika juhudi ya hivi punde kujaribu kufikia makubaliano ya kusitisha vita saa chache kabla ya muda wa mwisho wa kufikia makubaliano kuisha.

https://p.dw.com/p/1GGYp
Picha: AFP/Getty Images

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wamekutana pamoja na marais wa kanda hiyo ya Jumuiya ya ushirikiano wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD nchini Ethiopia.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema viongozi hao wa Sudan Kusini wanashinikizwa na Jumuiya ya kimataifa kutia saini makubaliano ya amani kabla ya leo kukamilika la sivyo wakabiliwe na hatari ya kuwekewa vikwazo.

Kiir ana mashaka iwapo amani itadumu

Rais Kiir ambaye aliwasili nchini Ethiopia jana jioni amesema ameshurutishwa kujiunga na mazungumzo hayo na kuonya kuwa haitawezekana kutia saini makubaliano ya kudumu au kamili ya amani hadi makundi yote ya upinzani yaweze kujiunga katika makubaliano hayo.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/dpa/P. Dhil

Kiir amesema na hapa namnukuu amani isiyoweza kuendelezwa haiwezi kusainiwa, ni sharti utie saini kitu ambacho unaridhia. Iwapo makubaliano hayo yanafikiwa hii leo na kesho tunarudi katika vita, basi tutakuwa tumefikia nini? mwisho wa kumnukuu.

Awali Kiir alikuwa amesema hatahudhuria mazungumzo hayo akilalamika kuwa haitawezakana kufikia makubaliano kamili kwasababu upande wa waasi umegawanyika.

Hata hivyo Rais Kenyatta alikuwa na imani kuwa mazungumzo waliyoyafanya hapo jana yako katika njia ya kufikia makubaliano. Mazungumzo hayo ya jana yalidumu hadi alfajiri ya leo na viongozi hao wanatarajiwa kurejea katika meza ya mazungumzo baadaye leo.

Maelfu ya watu wameuawa nchini Sudan Kusini katika vita ambavyo vimedumu kwa miezi ishirini sasa. Vita hivyo vilianza mwezi Desemba mwaka 2013 baada ya Kiir kumshutumu Machar ambaye alikuwa makamu wake wa Rais kuwa anapanga njama ya kumpindua madarakani na kuchochea mauaji ya kikabila.

Duru hii mpya ya mazungumzo ilianza tarehe sita mwezi huu ikisimamiwa na IGAD pamoja na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, China, Uingereza, Norway na Marekani.

Je makubaliano yataashiria mwanzo mpya?

Mazungumzo hayo yanayofanyika mjini Addis Ababa yanatafuta kuwashinikiza viongozi wa Sudan Kusini kukubaliana kugawana madaraka na kuunda serikali mpya.

Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek Machar
Kiongozi wa waasi Sudan Kusini Riek MacharPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Senosi

Mbali na Rais Kenyatta, rais wa Uganda Yoweri Museveni, rais wa Sudan Omar al Al Bashir na Waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn wanashiriki katika mchakato huo wa kutafuta amani Sudan Kusini.

Takriban makubaliano saba ya kusitisha mapigano k atika taifa hilo lililojinyakulia uhuru mwaka 2011 kutoka kwa Sudan yamefikiwa lakini kuvunjwa siku chache au saa chache baada tu ya kufikiwa.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Iddi Ssessanga