Viongozi wa Sahel na Ufaransa waapa kuongeza nguvu za jeshi
14 Januari 2020Viongozi wa Ufaransa na Afrika Magharibi wameapa kuongeza juhudi za pamoja za kijeshi katika ukanda wa Sahel ambao umeshuhudia ongezeko la vurugu na umwagikaji wa damu katika siku za hivi karibuni. Viongozi hao pia wametoa wito kwa Marekani kuunga mkono juhudi zao za kupambana na makundi ya itikadi kali za kiislamu.
Marais wa Mali, Burkina Faso, Chad, Niger na Mauritania wamefanya mazungumzo ya pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuzungumzia suala la usalama wa Sahel katika mkutano wa kilele uliofanyika katika mji wa kusini mwa Ufaransa wa Pau.
Mkutano huo unajiri wiki moja tu baada ya Niger kusema kuwa idadi ya vifo kutokana na shambulio la wanamgambo wa Kiislamu imeongezeka hadi watu 89, na kulifanya shambulio hilo kuwa baya zaidi nchini humo.
Kwa kauli moja, viongozi hao wamesisitiza kuwa wataungana kwa ajili ya kupambana na makundi ya kigaidi yanayowakosesha usingizi. Aidha, viongozi hao wa Afrika Magharibi wamesema kuwa wanaunga mkono uwepo wa jeshi la Ufaransa katika mataifa yao na kutoa wito wa msaada zaidi wa kimataifa.
Ufaransa kuongeza wanajeshi 220
Ufaransa ambayo ilitawala sehemu kubwa ya Afrika Magharibi ina wanajeshi 4,500 katika eneo la Sahel. Licha ya idadi hiyo, Ufaransa imekosolewa vikali na wakaazi wa Sahel kwa kushindwa kuwahakikishia usalama wao.
Viongozi hao wa Afrika Magharibi pia wameelezea umuhimu wa jeshi la Marekani huku kukiwepo hofu kuwa huenda Marekani ikapunguza idadi ya vikosi vyake vya usalama barani Afrika.
Kuhusu hofu hiyo, Rais Macron amesema "Natumai kuwa nitaweza kumshawishi Rais Donald Trump kuwa vita dhidi ya ugaidi katika eneo hili ni muhimu."
Macron ameongeza kuwa kwa wakati huu kipaumbele ni kupambana na wanamgambo wa Greater Sahara wenye ushirika na kundi la kigaidi la IS.
Naye Rais wa Burkina Faso Roch Marc Christian Kabora amesema ni dhahiri kuwa matokeo wanayoyapata licha ya juhudi zao za pamoja bado hazijafikia matarajio ambayo watu wao.
Haya yanajiri baada ya Baraza la usalama katika Ikulu ya Marekani kuandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa Marekani inaunga mkono kiukamilifu juhudi za Ufaransa, Afrika na jamii ya kimataifa kuimarisha usalama na kupambana na ugaidi katika eneo pana la Sahel.
Ufaransa na nchi tano katika eneo la Sahel zimekubaliana kuongeza idadi ya vikosi vya usalama katika mpaka wa Mali, Niger na Burkina Faso ili kuimarisha ulinzi maana wanamgambo wenye silaha wamekuwa wakivuka katika mipaka hiyo kwa urahisi.
Macron amesema mbinu za kijeshi ambazo watazitumia sasa zitaboresha zaidi ujasusi na hivyo basi kuwa rahisi kwa vikosi vya usalama kukabiliana na mashambulizi kutoka kwa wanamgambo hao.
Yamkini, mkutano mwengine kama huo utafanyika tena mnamo mwezi Juni nchini Mauritania ili kutathmini hali ilivyo.
Vyanzo: AP/APE