Mazungumzo ya kimyakimya kutafuta usitishaji mapigano
11 Juni 2021Baada ya kushindwa kupatikana ushindi wa kijeshi katika migogoro, nchi za Magharibi mwa Afrika zinaonesha kuingia kwenye mazungumzo ya kimyakimya na makundi ya itikadi kali.
Miaka miwili baada ya chifu wa kabila la Fulani, Djibril Dialo, kukimbia kaskazini mwa nchi yake Burkina Faso alikokuwa akiishi kufuatia vitisho vya kuuwawa vilivyotoka kwa wanamgambo wa makundi ya itikadi kali, amepokea ombi asilolitarajia la kumtaka arudi nyumbani na kushiriki kwenye mazungumzo ya amani na watu wale wale waliotaka kumuua.
Adama Oudraogo, ambaye ni meya wa mji anakotokea Diallo wa Thiou, alimpigia simu Januari kwenda kusaidia kusimamia mazungumzo ya kumaliza mashambulizi ya miaka kadhaa ya makundi ya itikadi kali dhidi ya wanamgambo wa eneo hilo na raia ambayo yamesababisha maelfu ya watu kulikimbia eneo hilo.
Diallo, ambaye ni chifu wa kijadi wa kabila la wafugaji la Fulani, alisema yuko tayari kurejea ikiwa kila mmoja yuko radhi.
Kwa miongo kadhaa, majeshi ya nchi za Afrika Magharibi na washirika wao kutoka jumuiya ya kimataifa wamekuwa wakipambana kuyazima makundi ya wanamgambo yanayoendesha hujuma zao katika eneo la ukanda wa Sahel, baadhi ya makundi hayo yakihusishwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu.
Lakini mapambano ya vikosi hivyo hayakuweza kupata mafanikio makubwa.
Mashambulizi dhidi ya raia bado yanashuhudiwa mara nyingi na sehemu kubwa bado inashikiliwa na wapiganaji kwa maneno mengine ni kwamba serikali haina udhibiti wa sehemu kubwa ya nchi.
Mamia ya wanajeshi wameuwawa tangu wanamgambo walilidhibiti eneo kubwa la Mali mnamo mwaka 2012.
Hivi sasa katika eneo kubwa linaloshuhudia uasi huko Burkina Faso na nchi jirani ya Mali, viongozi wa maeneo hayo wanatafuta njia za kukaa chini kimya kimya bila ya kutangaza rasmi kuzungumza na wanamgambo hao.
Mazungumzo ya kimyakimya
Serikali za nchi hizo hazikubali kuweka wazi kwamba kuna mazungumzo yanayofanyika lakini vyanzo vitano vinavyohusika kwenye mazungumzo hayo vimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba mamlaka zimekuwa zikiunga mkono juhudi hizo kimya kimya.
Mshirika wa kijeshi na koloni la zamani la nchi hizo,Ufaransa ambayo ina wanajeshi 5,100 kwenye ukanda huo inawaunga mkono wanajeshi wa eneo hilo ikisema wanamgambo watatumia fursa ya makubaliano ya kusitisha vita kujipanga upya,kujihami na kuandikisha wapiganaji.
Rais wa nchi hiyo Emmanuel Macron amesisitiza juu ya kutounga kwake mkono mazungumzo hayo. Siku ya Alhamis (Juni 10) aliwaambia waandishi habari kwamba wanajeshi wa Ufaransa hawatoendesha operesheni ya pamoja ya kijeshi na nchi ambazo zimeamua kukaa kwenye meza ya mazungumzo na makundi ambayo yanawapiga risasi na kuwauwa watoto, japokuwa kuna ishara za uhakika zinazoonesha kwamba kuwajongelea wanamgambo hao, huenda kunasaiduia kuzuia umwagikaji damu katika maeneo ambako hutokea sana mashambulizi.
Data zilizokusanywa na mpango ulioanzishwa nchini Marekani wa ACLED - unaofutilia migogoro inayohusisha silaha na matukio katika eneo la kaskazini, Sahel na jimbo la Burkina Faso la Boucle de Maouhoun, zinaonesha kwamba vifo vinavyotokana na migogoro ya umwagikaji damu vimepungua kwa kiwango kikubwa, ingawa mambo mengine kama opresheni za hivi karibuni za kijeshi huenda zikawa zimechangia kupunguwa huko.
Katika upande wa kaskazini, idadi ya vifo vilivyosababishwa na mapigano na vita dhidi raia imepungua kutoka asilimia 65 katika kipindi cha robo ya mwanzo ya mwaka 2020 hadi 26 katika robo ya mwanzo ya mwaka huu wa 2021.
Imeelezwa kwamba mikutano ya mwanzo ilifanyika Desemba kwa siri kwenye msitu ulioko nje wa eneo la mji wa Thiou kwenye jimbo la kaskazini nchini Burkina Faso.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef