Viongozi wa NATO wahitimisha mkutano wao wa kilele
11 Julai 2024Viongozi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO waliokusanyika mjini Washington, wanatarajiwa hivi leo kufanya mazungumzo na viongozi wa Japan, Korea Kusini, Australia na New Zealand, ambayo yatafuatiwa na mazungumzo zaidi na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyeahidiwa na muungano huo kupewa misaada zaidi ya kijeshi.
Mikutano hiyo inahitimisha mkutano wa kilele wa siku tatu wa NATO ulioanza Jumanne ambao ulikuwa pia fursa ya kusherehekea miaka 75 ya muungano huo wa kijeshi.
NATO itazungumza na nchi hizo nne za kanda ya Bahari ya Hindi na Pasifiki ambazo si wanachama wa jumuiya hiyo, lakini walialikwa ili kujadili masuala muhimu ya usalama na maslahi ya pamoja ya kikanda, katika dhamira ya kukabiliana na ushawishi wa China.
Soma pia: Viongozi wa NATO kukutana na Zelensky
Siku ya Jumanne na Jumatano, viongozi wa NATO walitangaza msaada zaidi wa kijeshi ili kuunga mkono juhudi za Ukraine za kukabiliana na uvamizi wa Urusi, ikijumuisha mifumo ya ulinzi wa anga, ndege za kivita chapa F-16 pamoja na ahadi ya kutumia dola bilioni 43 mwaka ujao. Viongozi hao walitangaza pia kuwa mustakabali wa Ukraine kuwa mwanachama wa NATO "kamwe hauepukiki."
Marekani kupeleka silaha nzito nchini Ujerumani
Marekani imetangaza itaanza kupeleka makombora ya masafa marefu nchini Ujerumani kuanzia mwaka 2026, hii ikiwa ni hatua muhimu ambayo washirika wa Jumuiya ya kujihami, NATO wamesema inalenga kudhibiti ongezeko la kitisho cha Urusi barani Ulaya.
Soma pia: Jeshi la Ujerumani lina utayari kubeba dhamana NATO?
Chini ya makubaliano hayo, Marekani itapeleka kwa awamu silaha nzito kabisa ambazo haijawahi kuzipeleka barani Ulaya tangu enzi za Vita Baridi, hili likichukuliwa kama onyo la wazi kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Hatua hiyo pengine isingeliweza kutekelezeka kutokana na makubaliano ya Nyuklia kati ya Marekani na uliokuwa Umoja wa Sovieti yaliyotiwa saini mwaka 1987 lakini makubaliano hayo yaliyovunjika mwaka 2019.
NATO yahofia uwezekano wa shambulio la Urusi
Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi wa NATO walisisitiza kuwa hawawezi kupuuza uwezekano wa shambulio la Urusi dhidi ya nchi mojawapo washirika.
Rais Joe Biden aliwakaribisha hapo jana washirika wake wa NATO kwenye dhifa ya chakula cha jioni katika Ikulu ya White House ili kusherehekea kile alichokiita "muungano mkubwa zaidi ambao ulimwengu haujawahi kuushuhudia." Wakati huohuo Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema:
"Na kama mnavyojua, katika tamaduni zote na wakati wote, kushiriki mlo, kuwa pamoja, kupata chakula cha jioni ni mojawapo ya ishara kubwa ya uaminifu, urafiki na udugu. Na usiku wa leo, sisi ni familia kubwa ya NATO, tukiwa pamoja na marafiki zetu wa karibu, marafiki zetu kutoka Ukraine na kutoka eneo la Asia-Pasifiki. Hakika, hiki ni chakula cha jioni kwa familia hii kubwa."
Soma pia: Washirika wa NATO wakubaliana kukabiliana na kitisho cha Urusi na kuendelea kuisaidia Ukraine
Katika hotuba yake siku ya Jumanne Biden alisisitiza kwamba NATO imekuwa na "nguvu zaidi kuliko hapo awali" na kwamba kutokana na msaada kamili na wapamoja wa jumuiya hiyo, Ukraine inaweza na bila shaka itamshinda rais wa Urusi Vladimir Putin.
(Vyanzo: Mashirika)