Viongozi wa eneo la Maziwa Makuu waijadili Congo
9 Oktoba 2018Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa asubuhi ya leo baada ya mkutano huo jana jioni, viongozi hao wameazimia kuendelea kuushawishi utawala wa rais wa Congo, Joseph Kabila, kuimarisha juhudi za kukomesha vitendo vya kigaidi na mateso kwa binadamu hasa katika eneo la Mashariki mwa Congo.
Kwa mujibu wa azimio lao la kukomesha mizozo na mateso kwa raia katika eneo la maziwa makuu hasa katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, viongozi na wajumbe wa ngazi za juu kutoka mataifa 11 walikuwa na mkutano wao wa awamu ya tisa chini ya mkataba wa muundo wa amani, usalama na ushirikiano uliosainiwa mwezi Februari mwaka 2013. Chini ya mkataba huo nchi hizo zilizo na mipaka na Congo zinatarajiwa kuisaidia nchi hiyo kuleta amani ndani ya nchi, jambo ambalo litachangia katika kuimarisha amani katika kanda hiyo ya maziwa makuu. Rais Museveni amekabidhiwa Uwenyekiti wa jopo hilo.
Madini chanzo cha mzozo Congo
Hivi karibuni kumekuwepo na mjadala kuwa mizozo, vita na ukiukaji wa haki za binadamu hasa mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kunatokana utajiri mkubwa wa madini. Biashara haramu za madini hayo ikitajwa kuwa chanzo cha mapato kwa makundi ya waasi na hata kuhusishwa wanajeshi wa kulinda amani wa umoja mataifa.
Rais wa Zambia, Edgar Lungu, ambaye aliongoza ujumbe wa Jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, SADC, alirudia wito kwa kuwataka wadau wote kukabiliana na hali hiyo.
Ikumbukwe kuwa makundi mbalimbali ya waasi dhidi ya tawala za Rwanda, Uganda na hata Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yenyewe yanaendelea na harakati zao katika sehemu hiyo. Kwa sasa kuzuka kwa janga la ebola kumesababisha hofu mpya kutokana na ukosefu wa uthabiti katika eneo hilo, hali inayosababisha matatizo makubwa kwa watalamu wa tiba kuudhibiiti ugonjwa huo.
Mkutano huo uliohudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Umoja mataifa, Umoja wa Afrika na mashirikisho ya kibiashara umeorodhesha maazimio kadhaa ili kufanikisha juhudi za kuleta amani na usalama nchini Congo.
Lubega Emmanuel DW Kampala.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman