1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Marsabit walaumiwa kufadhili machafuko

Admin.WagnerD7 Juni 2021

Viongozi katika jimbo la Marsabit nchini Kenya wamelaumiwa na serikali nchini humo, inayodai kwamba wamekuwa wakifadhili mapigano ya kikabila yanayotokea mara kwa mara ili kujiimarisha kisiasa.

https://p.dw.com/p/3uWDA
Wassermangel in Marsabit, Kenia
Picha: Wassermangel , Wasser, Dürre, Trockenheit, Afrika, Marsabit, Kenia

Mamlaka nchini Kenya zinawalaumu viongozi wa Marsabit kaskazini mwa nchi hiyo kwa ongezeko la uhasama na vita vya kikabila kila wakati. Kwa mujibu wa wizara ya usalama, viongozi kutoka jimbo hilo wamekuwa wakilifumbia macho swala la usalama na kutumia mizozo ya kijamii kujiendeleza kisiasa. 

Ukosefu wa usalama katika jimbo la Marsabit ambao umeshuhudiwa kwa miongo kadhaa sasa, umehusishwa na wahalifu ambao wamekuwa wakipigana kwa niaba ya jamii zao. Lakini wahalifu hao, kulingana na wizara ya usalama, wamekuwa wakipata usaidizi kutoka kwa viongozi wa jamii zao kama hatua ya kuwa na ushawishi katika ngome zao.

Katika mkutano na wanahabari, mrakibu wa usalama kanda za juu mashariki mwa Kenya, Isaiah Nakoru, amesema anasikitishwa na viongozi kutoka jimbo hili la Marsabit kuendelea kusalia kimya licha ya misururu ya mauaji ambayo yamekuwa yakiripotiwa katika kaunti hii.

Kenia
Eneo la Marsabit linaloonekana kugubikwa na utulivu, ingawa kila wakati kumekuwa kukiripotiwa mapigano.Picha: DW

Aidha, Nakoru alidai kuwa baadhi ya watu wenye ushawishi kutoka Marsabit wamekuwa wakijihusisha na ulanguzi wa silaha haramu hali ambayo pia imechangia ukosefu wa usalama hapa.

"Kuna watu wanaendelea kuleta bunduki haramu na kuwauzia wananchi na hata tumewakamata wengine juzi. Kila jamii ina wakora wake, yaani militias wake, na si uongo na viongozi watueleze, kama wako wanawaweka ya nini.” aliongeza.

Na kama hatua ya kupambana na wahalifu hao, wizara ya usalama kwa mara nyingine imetangaza kuzuwia matumizi ya Msitu wa Marsabit, ambao umebainika kutumika kama maficho ya wahalifu baada ya kufanya mauaji na wizi wa mifugo.

Wakati huo huo, wizara hiyo imetangaza mpango wa kuwahusisha machifu kutoka maeneo yote ya kaunti hii kusaidia katika mapatano ya kijamii. Machifu hao wametwikwa majukumu ya kuhamasisha wananchi umuhimu wa amani na athari za vita vya kikabila:

Nakoru alisema "Machifu wataanza kuzunguka kuanzia leo jumatatu wakiwaeleza wananchi umuhimu wa amani ,jinsi ya kurudiana,kusameheana.Kuna watu waliyatoroka makaazi yao na tunataka warudi makwao.Wazee na machifu wote watashirikana ili kumaliza haya maswala”

Jimbo la Marsabit katika siku za hivi karibuni limeripoti vita vya kikabila ambapo watu wasiopungua kumi wameuawa chini ya kipindi cha mwezi mmoja.

Sikiliza zaidi: 

Chanzo cha migogoro ya makabila Marsabit

Michael Kwena/DW Marsabit