Viongozi wa makundi ya Hamas na Fatah nchini Palestina waapa kukomesha machafuko
5 Oktoba 2005Kufuatia kuuwawa kwa wapalestina watatu katika mapigano makali kati ya polisi na kundi la Hamas, viongozi wa makundi ya Hamas na Fatah nchini Palestina, wameahidi kutoyatumia machafuko katika kuyasuluhisha matatizo yanayowakabili wapalestina.
Kamanda wa polisi na raia wawili waliuwawa katika mapigano kati ya maofisa wa polisi na wapiganaji wa kundi la Hamas. Watu 50 walijeruhiwa baada ya wanamgambo kujaribu kukishambulia kituo cha polisi mda mfupi baada ya mapigano hayo.
Farouk Kaddoumi, kiongozi wa kundi la Fatah amesema viongozi wa makundi hayo, walio uhamishoni, waliafikiana mjini Damascus nchini Syria, kwamba mazungumzo yanatakiwa kuwa njia ya pekee ya kuitanzua mizozo kati ya makundi hayo mawili.
Akizungumzia kuhusu uamuzi uliopitishwa katika mkutano huo, Kadduni amesema viongozi wote wamekubaliana kutoa mwito wa pamoja kwa makundi yote nchini Palestina kupiga marufuku matumizi ya mtutu wa bunduki katika kuyatatua matatizo ndani ya Palestina. Aliongeza kwamba viongozi hao wamekubaliana kujiepusha mbali na ushawishi wa kisiasa na vyombo vya habari ambao unaweza kuvuruga umoja wa taifa na masilahi ya raia.
Kiongozi wa kundi la Hamas, Khaled Meshaal, amekubaliana na mwito huo lakini akalitetea kundi lake akisema lina haki ya kuipinga Israel kuyakalia maeneo ya Palestina na wakati huo huo kushiriki katika juhudi za kisiasa nchini humo. Meshaa hata hivyo amepinga vita vya wenyewe kwa wenyewe akisema ni mwiko kwa mpalestina kuimwaga damu ya mpalestina mwengine.
Kundi la Hamas limewatetea wapiganaji wake waliohusika katika mapigano na polisi likisema walifanya hivyo kujilinda baada ya kushambuliwa kwa risasi na maofisa wa polisi. Pia walitaka kuyalinda makazi ya wanasiasa wa Hamas ambayo pia yalishambuliwa na polisi. Meshaal amesema kundi la Hamas linataka kuitatua mizozo iliyopo kwa njia ya mazungumzo, lakini akayalaumu mataifa ya kigeni, ambayo hakuyataja, yanayochochea machafuko kati ya makundi mbalimbali nchini Palestina.
Wakati haya yakiarifiwa, wanajeshi wa Israel wamempiga risasi na kumuua mwanamke aliyemdunga kisu mwanajeshi wa kike wa Isreal kwenye kituo cha ukaguzi katika ukingo wa magharibi hapo jana. Kundi la wanamgambo la Al- Aqsa limetangaza kwamba mwanamke huyo alikuwa njiani kwenda kufanya shambulio la bomu la kujitoa muhanga nchini Israel.
Haifa Hindiya, mwenye umri wa miaka 36, na mama wa watoto watano, alikuwa ametumwa kwenda kulipiza kisasi mauaji ya wanamgambo wawili wa kundi hilo yaliyofanywa na wanajeshi wa Israel katika eneo la ukingo wa magharibi.
Katika taarifa yake kundi la Al-Aqsa lilisema haliutambui wala kuuheshimu mkataba wa kusitisha mapigano na litaendelea kuipinga hatua ya Israel kuyakalia maeneo ya wapalestina na kuwashambulia wanajeshi wa Israel.
Kamanda wa jeshi la Israel amesema mwanamke huyo alipigwa na kuanguka chini baada ya kumjeruhi mwanajeshi wa kike wa Israel na kwamba wanajeshi walimpiga risasi alipoinuka na kujaribu kuwashambulia akiwa na kisu chake mkononi. Ameongeza kusema mwanamke huyo hakuwa na silaha zozote zinazodhihirisha alikuwa na njama ya kufanya shambulio la kujitoa muhanga.
Israel imelifunga eneo la ukingo wa magharibi baada ya likizo ya kiyahudi kuanza mnamo Jumatatu wiki hii. Kuimarishwa kwa usalama katika eneo hilo kunawaathiri wapalestina wachache ambao hupata kibali cha kuitembelea Israel.
Mapigano yanayoendelea hivi sasa yanayazika matumaini kwamba kuondoka kwa Israel kutoka ukanda wa Gaza mwezi uliopita kutafungua njia ya amani kati ya Israel na Palestina.