Viongozi wa kikanda waimarisha vita dhidi ya Boko Haram
8 Oktoba 2014Pia wataweka kituo cha kijeshi cha kupambana na wanamgambo hao ambao harakati zao za uasi zimesambaa hadi nje ya mipaka ya Nigeria. Uasi wa Boko Haram uliodumu miaka mitano sasa wa kutaka kuunda taifa la kiislamu umesababisha vifo vya maelfu ya watu na unatishia amani na utulivu wa mataifa ya maeneo ya Afrika Magharibi na Kati.
Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, kundi hilo limebadili mbinu zake za kufanya misururu ya mashambulizi, uvamizi, kuwateka nyara watu na kuanza sasa kujaribu kuyateka maeneo ya mbali na vijijini karibu na mpaka wa Cameroon, labda kwa kutiwa motisha na harakati za aina hiyo zinazofanywa na wanamgambo wa Kisunni nchini Iraq na Syria. Wanamgambo hao pia wamefanya uvamizi nchini Niger na Chad, na maafisa wanahofia kuwa mashambulizi yao yataendelea kusambaa kama hayatadhibitiwa.
Viongozi wanne wa nchi pamoja na wawakilishi wa rais wa Cameroon wamesema baada ya mkutano wao ulioandaliwa katika mji mkuu wa Niger, Niamey hapo jana, kuwa kituo cha kuongoza mapambano ya kikosi cha mataifa ya kanda hiyo ambacho tayari kimeundwa, kikiongozwa na mkuu wa jeshi kitaanza kufanya kazi mnamo Novemba 20.
Waziri wa ulinzi wa Niger Mahamadou Karidjo amesema kuwa viongozi wa mataifa hayo ya kikanda wanasikitishwa na ongezeko la vitendo vya kinyama na kigaidi vinavyofanywa na kundi hilo la Boko Haram dhidi ya raia na vikosi vya usalama nchini Nigeria na jirani zake.
Viongozi hao walikubaliana kukamilisha mipango ya kuwatuma wanajeshi ambao nchi wanachama ziliahidi kutoa ili kuunda jeshi hilo la pamoja la kimataifa katika mipaka ya nchi hiyo ifikapo Novemba mosi.
Mnamo mwezi Julai, Niger, Chad, Nigeria na Cameroon ziliahidi kutoa wanajeshi 700 kila nchi ili kuunda kikosi cha pamoja cha kimataifa kupambana na kundi hilo lenye makao yake nchini Nigeria, ambalo limewaua zaidi ya watu 10,000 tangu mwaka wa 2009.
Benin, jirani ya Nigeria katika upande wa magharibi, ambayo mpaka wake unaanzia bahari ya Atlantic hadi kaskazini ya eneo la sahel, pia imetakiwa kukipeleka kikosi cha jeshi katika mpaka wake na Nigeria.
Mkutano huo wa Niamey, unafuatia mkutano wa kilele ulioandaliwa mwezi Mei mjini Paris ambapo viongozi waliahidi kuimarisha ushirikiano wao katika vita dhidi ya Boko Haram baada ya kundi hilo kuwateka nyara zaidi ya wasichana 200 wa shule na kutishia kuvuruga usalama wa eneo hilo zima.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Oumilkheir Hamidou