1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa kikabila Darfur watangaza kuiunga mkono RSF

6 Julai 2023

Viongozi wa makabila ya Waarabu kutoka eneo la magharibi mwa Sudan la Darfur wametangaza utiifu wao kwa wanamgambo wa RSF wanaopambana na jeshi.

https://p.dw.com/p/4TUzU
Sudan Soldaten der RSF Truppe
Picha: Rapid Support Forces/AFP

Wachambuzi wanaonya kuwa tangazo la viongozi hao wa makabila ya Waarabu linaweza kuuzidisha mzozo uliodumu kwa miezi kadhaa sasa na kusababisha vifo vya watu 3000.

Katika ujumbe wa vidio uliotolewa mapema wiki hii, viongozi kutoka makabila saba makuu katika jimbo la Darfur wamehimiza jamii zao kupambana na jeshi badala ya kuwaona wanamgambo wa RSF kama maadui.

Vita kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza vikosi vya RSF vimesababisha maafa katika eneo la Darfur, na wataalam wanahofia kuongezeka kwa mgawanyiko wa kikabila unaweza kusababisha ghasia zaidi.

Wengi wanahofia kujirudia kwa historia ambapo kundi la wanamgambo wa RSF lenye chimbuko lake kutoka kwa wanamgambo wa kiarabu na wanaoogopwa mno wa Janjaweed ambao walifanya ukatili mkubwa dhidi ya makabila madogo ya Waarabu huko Darfur kuanzia mwaka 2003.