Viongozi wa Kiarabu wataak hatua zichukuliwe dhidi ya Iran
31 Mei 2019"Kutokuwapo kwa msimamo mkali na madhubuti kukabiliana na vitendo hivi vya kigaidi vya utawala wa Iran katika eneo hili kumesababisha Iran iendelee na hali hiyo na pia kuongezeka ambako tunakuona," Mfalme Salman amesewaambia viongozi wa mataifa ya kiarabu.
"Hivi leo tunakabiliwa na kitisho katika usalama wa mataifa ya kiarabu, operesheni za uharibifu zinazolenga meli za kibiashara karibu na eneo la maji la Umoja wa Falme za Kiarabu , kushambuliwa vituo viwili vya kusukuma mafuta nchini Saudi Arabia kulikofanywa na wanamgambo magaidi wanaoungwa mkono na Iran.
Mapema mwezi huu , meli nne za kibiashara zilihujumiwa nje ya pwani ya Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, na ndege zisizokuwa na rubani zenye mabomu zilishambulia vituo viwili vya kusukumia mafuta katika bomba la mafuta katika jimbo la Riyadh nchini Saudi Arabia.
Mei 18, Mfalme Salman aliitisha mkutano wa dharura wa jumuiya ya mataifa ya Kiarabu kujadili mashambulio hayo, ambayo Marekani imeitwisha jukumu Iran, hasimu wa kikanda wa Saudi Arabia. Iran inakana shutuma hizo.
Taarifa ya viongozi wa mataifa ya kiarabu inayoshutumu Iran kwa kuingilia masuala ya mataifa ya kanda hiyo yamekanushwa vikali na Iran leo, ambapo msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ametupilia mbali shutuma hizo na kusema ni madai yasiyo na msingi.
Matumizi mabaya ya mwezi wa Ramadhan
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran Abbas Mousavi ameliambia shirika la habari la nchi hiyo ISNA kuwa Saudi Arabia imetumia mwezi wa Ramadhani na mji mtakatifu wa Mecca kupata manufaa ya kisiasa ili kuieleza dunia kuhusu madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran. Ameongeza kwamba lengo kuu la mataifa ya Kiislamu na Kiarabu linapaswa kuwa ukombozi wa Wapalestina, na sio kulumbana.
Hata hivyo rais wa Iraq Barham Salih amewataka viongozi wa mataifa ya Kiarabu kutafakari kabla ya kuchukua hatua dhidi ya Iran.
"Ndugu zangu, katikati ya nyakati hizi tete na matukio yanayotokea kwa kasi na kanda hii yenye hali ya wasiwasi na mazingira ya dunia yenye wasi wasi mkubwa na vitisho, tunashuhudia mbele ya macho yetu kuongezeka kwa mzozo wa kikanda na kimataifa ambao unaweza kugeuka kuwa vita ambavyo vitatuhusu sisi wote. Iwapo mzozo huu hautashughulikiwa vizuri, tutakabiliwa na hatari ya makabiliano kikanda na kimataifa ambayo yataleta maafa kwa nchi zetu."
Mfalme wa Saudi Arabia amerudia leo kusema kwamba nchi hiyo wakati wote itanyoosha mkono kwa ajili ya ushirikiano na majadiliano na mataifa mengine ya kanda hiyo na duniani ili kuhimiza maendeleo na ufanisi na kufikia amani ya kudumu.