Waziri mkuu Haiti akubali kuandaa uchaguzi katikati ya 2025
29 Februari 2024Hayo ni wakati jumuiya ya kimataifa ikijitahidi kuchangisha fedha kwa ajili ya kupeleka kikosi cha kigeni cha kupambana na machafuko yanayosababishwa na magenge ya wahalifu nchini humo.
Wanachama wa jumuiya ya kikanda ya kiuchumi - CARICOM wametoa taarifa baada ya mkutano wa kilele wa siku nne nchini Guyana wakisema Henry amekubali kuwa ipo haja ya kuandaa uchaguzi na kushirikiana na upinzani na mashirika ya kijamii ili kutimiza lengo hilo.
"Ni muhimu sana kwamba nchi za Karibia, ujumbe wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa na watu mashuhuri wa Caricom washiriki katika upatanishi kati ya makundi ya kisiasa ya Haiti," alisema Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, mmoja wa waliohudhuria mkutano huo.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetoa ombi la kibinaadamu kwa mwaka huu na unatafuta dola milioni 674. Zaidi ya nusu ya fedha hizo zitatumika kununua chakula. Mratibu wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti Ulrika Richardson amesema hali ya machafuko ni mbaya mno nchini humo.