Viongozi wa G8 wakubaliana juu ya vikwazo dhidi ya serikali ya Mugabe
9 Julai 2008TOYAKO
Viongozi wa nchi za G8 wanaokutana nchini Japan wametoa sauti moja ya kulaani uchaguzi wa hivi karibuni nchini Zimbabwe uliomrudisha tena madarakani rais Robert Mugabe.Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema viongozi hao wakuu wa dunia wamekubaliana juu ya kuwekewa vikwazo zaidi dhidi ya serikali ya rais Robert Mugabe.Amesema msimamo huo umefikiwa kuonyesha umoja katika jumuiya ya kimataifa kupinga maovu wanayoyakabili wazimbabwe na kuendelea kubakia madarakani rais Robert Mugabe kwa njia haramu. Aidha viongozi wa G8 wamekubaliana juu kupunguza kwa nusu viwango vya utoaji wa gesi ya sumu kufikia mwaka 2050 ili kukabiliana na ongezeko la ujoto duniani.Hata hivyo mpango huo haujafafanuliwa vizuri katika taarifa iliyotolewa hapo jana na viongozi hao lakini huenda ukawekwa wazi hii leo wakati watakapokutana na viongozi wa nchi zinazoendelea zinazojulikana kama G5 ,China,India,Afrika Kusini,Mexico na Brazil. Nchi hizo tayari zimeshawakosoa viongozi wa G8 kwa kushindwa kuchukua hatua za kutosha juu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Mkutano wa Japan ambao unaingia siku yake ya mwisho hii leo unatarajiwa kulenga zaidi kuhusu masuala ya kiuchumi.