1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJapan

Viongozi wa G7 waionya China dhidi ya kujitanua kijeshi

20 Mei 2023

Viongozi wa kundi la mataifa tajiri la G7 wameionya China dhidi ya kutanua shughuli zake za kijeshi kwenye kanda ya Asia na Pasifiki lakini wamesisitiza pia dhamira ya kuwa na mahusiano imara na utawala wa mjini Beijing.

https://p.dw.com/p/4RbVj
Viongozi wa kundi la G7 wakiwa Hiroshima, Japan
Viongozi wa kundi la G7 wakiwa Hiroshima, Japan Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kwenye tamko la mwisho lililotolewa baada ya mkutano wa kilele wa kundi la G7 uliofanyika kwenye mji wa Hiroshima nchini Japan, viongozi wa mataifa hayo wameorodhesha masuala kadhaa yanayowatia wasiwasi kutokana na shughuli za kijeshi na kiuchumi za China.

Wametahadharisha dhidi ya kujitanua kijeshi kwa China kwenye eneo la bahari ya kusini na kurejea msimamo wao kwamba "amani na uthabiti" kwenye ujia wa bahari wa Taiwan ni suala muhimu kwa usalama wa dunia.

Hata hivyo wamesema wako tayari kushirikiana na Beijing na kwamba misimamo wanayochukua hailengi kuidhuru China wala kulemaza maendeleo ya kiuchumi ya dola hiyo ya mashariki ya mbali.